Pendekezo la mazungumzo mapya ya nyuklia linaonesha udhaifu wa Ulaya
(last modified Sat, 18 Jan 2020 07:37:54 GMT )
Jan 18, 2020 07:37 UTC
  • Pendekezo la mazungumzo mapya ya nyuklia linaonesha udhaifu wa Ulaya

Balozi wa Iran mjini Paris amesema pendekezo la kutaka kufanyika mazungumzo mapya kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran linaonesha udhaifu wa Ulaya na ni dhihirisho wazi kuwa nchi hizo zina uepesi wa kuvunja mapatano.

Akitoa radiamali yake baada ya nchi kadhaa za Ulaya kutoa pendekezo la kujadiliwa upya JCPOA kama anavyoshinikiza mara kwa mara Rais Donald Trump wa Marekani, Bahram Qasemi amesema hakuna mtu mwenye mantiki na mwenye ufahamu juu ya JCPOA ana shaka kuwa mapatano hayo ni bora zaidi na yenye suluhu inayotekelezeka.

Katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Bahram Qasemi, Balozi wa Iran nchini Ufaransa amesema pendekezo hilo la Ulaya limetokana na mashinikizo kutoka upande fulani.

Hii ni katika hali ambayo, toleo la siku ya Jumatano ya tarehe 15 Januari la gazeti la Washington Post lilizinukuu duru za kuaminika ndani ya Umoja wa Ulaya zikiripoti kuwa, serikali ya Trump imewatishia maafisa wa nchi tatu za Ujerumani, Ufaransa na Uingereza (Troika ya Ulaya) kwamba Marekani itayawekea ushuru mpya wa asilimia 25 magari yanayotoka nchi hizo, vyenginevyo watekeleze utaratibu wa kusuluhisha mgogoro katika JCPOA, unaojulikana kama "Trigger Mechanism."

Wakuu wa Troika ya Ulaya

Licha ya kutumbukia kwenye mashinikizo hayo ya Trump ya kushinikiza kufanyika mazungumzo mapya ya nyuklia, lakini nchi hizo za Ulaya zinadai kuwa haziungi mkono sera ya Washington ya kuiwekea Iran mashinikizo ya hali ya juu.

Baada ya nchi za Ulaya kushindwa kudhamini maslahi ya Iran kwenye makubaliano hayo baada ya Marekani kujiondoa kwayo, Iran iliamua kuchukua hatua kupitia awamu tano zilizopishana kwa muda wa siku 60 kila moja, za kupunguza uwajibikaji wake katika JCPOA.

 

Tags