Wanaharakati wanaopinga vita: Vikwazo ni jinai ya kivita
Washiriki katika kikao cha kukumbuka maangamizi ya kizazi kilichofanyika jana mjini London Uingereza wamesema kuwa vikwazo ni miongoni mwa siasa za Marekani katika uwanja huo ambazo ni sawa na jinai za kivita.
Katika kikao hicho kilichohuhudhuriwa na wasomi wachambuzi wa masuala ya kisiasa, wanaharakati wanaopinga vita, watetezi wa haki za binadamu na wamiliki wa vyombo vya habari; watoa hotuba walivitaja vikwazo kuwa ni wenzo unaotumiwa na madola ya kibeberu kuimarisha ubeberu wao duniani.
Profesa Said Khan Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Detroit jimboni Michigan nchini Marekani ameashiria katika hotuba yake kuhusu maangamizi ya kizazi yaliyofanywa na Marekani huko Iraq baada ya kupinduliwa dikiteta wa nchi hiyo Saddam Hussein.
Naye Profesa Ramon Grosfoguel Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Berkeley cha California nchini Marekani amesema kuwa Marekani na utawala wa Kizayuni baada ya Vita vya Pili vya Dunia zilitumia zaidi wenzo wa vikwazo kutekeleza maangamizi ya kizazi hata hivyo kamwe hazikuadhibiwa au kuhukumiwa na jamii ya kimataifa.
Shughuli maalumu ya kumbukumbu ya kulaani "maangamizi ya kizazi" kwa ubunifu wa Kamisheni ya Kiislamu ya Haki za Binadamu ya Uingereza hufanyika jijini London kila mwaka mwishoni mwa mwezi Januari tangu mwaka 2010 hadi sasa.