Russia: tutapinga kurejeshwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amevitaja vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran kuwa kinyume cha sheria na kueleza kuwa Moscow itapinga juhudi zozote kwa lengo la kuirejeshea Tehran vikwazo vya Umoja wa Mataifa.
Mikhail Bogdanov amelaani hatua ya Marekani ya kuziwekea vikwazo baadhi ya nchi kutokana na nchi hizo kushirikiana na Iran na kuvitaja kuwa kinyume cha sheria. Bogdanov ameongeza kuwa Russia itapinga kurejeshwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran na umoja huo haupasi kutumiwa na baadhi ya nchi kama mwanasesere.
Mike Pompeo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani juzi alisema kuwa nchi hiyo imewawekea vikwazo watu na taasisi 13 huko China, Iraq, Russia na Uturuki. Kuhusu kikao cha jana cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA huko Vienna, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza pia kwamba kikao hicho kimetaka kuendelezwa mzunguko wa washiriki katika mchakato wa INSTEX. Amesema katika siku chache zijazo uamuzi utachukuliwa kuhusu suala hilo.
Vienna mji mkuu wa Austria jana Jumatano ulikuwa mwenyeji wa kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA katika ngazi ya Manaibu na Wakurugenzi wa Kisiasa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na wa kundi la 4+1 linaloundwa na Ujerumani, Ufaransa, Russia, China na Uingereza pamoja na Umoja wa Ulaya. Taarifa ya mwisho ya kikao hicho imeeleza kuwa wanachama wa mapatano ya JCPOA wamekiri kuwa vikwazo vya Marekani vinaizuia Iran kunufaika kikamilifu na maslahi ya mapatano hao na mijadala ya kiufundi na kitaalamu kuhusu suala hilo itaendelea.