Bunge la Juu ya Uingereza lataka kuondolewa vikwazo Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i60380-bunge_la_juu_ya_uingereza_lataka_kuondolewa_vikwazo_iran
Mwenyekiti wa Kamati ya Uhusiano wa Kimataifa na Ulinzi ya Bunge la Juu la Uingereza (House of Lords) amesema anaunga mkono miito inayotolewa na maafisa wa nchi za Ulaya na Marekani za kutaka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iondolewa vikwazo, katika kipindi hiki ambapo Iran inaendelea kukabiliana na maambukizi makubwa ya virusi vya Corona.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 15, 2020 03:39 UTC
  • Bunge la Juu ya Uingereza lataka kuondolewa vikwazo Iran

Mwenyekiti wa Kamati ya Uhusiano wa Kimataifa na Ulinzi ya Bunge la Juu la Uingereza (House of Lords) amesema anaunga mkono miito inayotolewa na maafisa wa nchi za Ulaya na Marekani za kutaka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iondolewa vikwazo, katika kipindi hiki ambapo Iran inaendelea kukabiliana na maambukizi makubwa ya virusi vya Corona.

Katika barua yake kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ofisi ya Jumuiya ya Madola ya Uingereza, Baroness Anelay, Mwenyekiti wa Kamati ya Uhusiano wa Kimataifa na Ulinzi ya Bunge la Juu la UK ameitaka serikali ya London kufanya kila liwezekanalo ili kuhakikisha kuwa, pendekezo hilo la maafisa wa Uingereza na Marekani la kuondolewa Iran vikwazo linatekelezwa.

Anelay amesema katika barua hiyo kuwa, vikwazo hivyo vinapaswa kuondolewa ili kuruhusu biashara ya kibinadamu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati huu wa kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 (Corona).

Kadhalika Mwenyekiti wa Kamati ya Uhusiano wa Kimataifa na Ulinzi ya Bunge la Juu la Uingereza ameitaka serikali ya London mbali na kuhakikisha pendekezo hilo la kundolewa Iran vikwazo linatekelezwa, lakini pia inaziasa pande zote za makubaliano ya nyuklia ya Iran (JCPOA) zinaunga mkono jambo hilo.

US imeendelea kushadidisha vikwazo vyake dhidi ya Iran licha ya janga la Corona

Wiki iliyopita, wanadiplomasia 24, mawaziri wa zamani pamoja na maafisa wa kijeshi wa baadhi ya nchi walimuandikia barua Rais Donald Trump wa Marekani wakimtaka aiondolee Iran baadhi ya vikwazo hasa wakati huu wa mlipuko wa virusi vya Corona. 

Taasisi za kimataifa na nchi mbali mbali duniani zimeendelea kulaani hatua ya upande mmoja ya Marekani, ya kuendelea kutumia vikwazo haramu na visivyo vya kibinadamu kudhuru afya na maisha ya wananchi wa Iran.