Marekani yakiri: Ni kweli tumeua raia katika shambulizi la anga Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i60652-marekani_yakiri_ni_kweli_tumeua_raia_katika_shambulizi_la_anga_somalia
Kamandi ya Jeshi la Marekani barani Afrika AFRICOM imekiri kuwa raia wawili wa Somalia waliuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika hujuma yake ya anga mapema mwaka jana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 28, 2020 02:49 UTC
  • Marekani yakiri: Ni kweli tumeua raia katika shambulizi la anga Somalia

Kamandi ya Jeshi la Marekani barani Afrika AFRICOM imekiri kuwa raia wawili wa Somalia waliuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika hujuma yake ya anga mapema mwaka jana.

Kamanda wa AFRICOM, Jenerali Stephen Townsend alikiri hayo jana Jumatatu katika ripoti na kusema, "kwa bahati mbaya, raia wawili waliuawa na wengine watatu walijeruhiwa katika shambulizi la anga la Februari 2019. Tunasikitika sana hili lilitokea."

Shambulizi hilo lilitokea katika mji wa Kunyo Barrow katika eneo la Lower Shabelle, ambapo AFRICOM inadai kuwa ilikusudia kuua wanachama wawili wa genge la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda.

Hii ni katika hali ambayo, mapema mwezi huu, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilisema jeshi la Marekani linaendelea kuua raia wasio na hatia katika mashambulizi yake ya anga nchini Somalia.

Raia ni wahanga wakuu wa hujuma za anga za US nchini Somalia

Amnesty ililaani mauaji ya raia wawili wa Somalia na kujeruhiwa wengine watatu katika shambulizi la drone za Marekani mwezi Februari mwaka huu katika mji wa Jilib yapata kilomita 112 kusini mwa Kismayo na katika kijiji cha Kumbareere, umbali wa kilomita 10 kutoka mji huo wa Jilib katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Utafiti uliofanywa hivi karibuni na asasi isiyo ya kiserikali ya Hiraal yenye makao makuu yake mjini Mogadishu ulibainisha kuwa, mashambulizi ya anga yanayofanywa kila uchao na Marekani nchini Somalia yameshindwa kulitokomeza au hata kulidhoofisha kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab na badala yake yamekuwa na taathira hasi kwa raia wa kawaida.