Umoja wa Ulaya: Tumo katika kushuhudia kusambaratika nguvu za Marekani duniani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i61214-umoja_wa_ulaya_tumo_katika_kushuhudia_kusambaratika_nguvu_za_marekani_duniani
Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amegusia kumalizika zama za udhibiti wa kila kitu wa Marekani duniani na ameutaka Umoja wa Ulaya kubuni mikakati na stratijia mpya na makini za kuamiliana na China.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 25, 2020 22:26 UTC
  • Umoja wa Ulaya: Tumo katika kushuhudia kusambaratika nguvu za Marekani duniani

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amegusia kumalizika zama za udhibiti wa kila kitu wa Marekani duniani na ameutaka Umoja wa Ulaya kubuni mikakati na stratijia mpya na makini za kuamiliana na China.

Joseph Borrel alisema hayo jana na kuongeza kuwa, kuenea ugonjwa wa COVID-19 inaweza kuwa nukta muhimu sana ya kubadilika mlingano wa nguvu za Magharibi na Mashariki.

Mkuu huyo wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya pia amesema, katika mabadiliko hayo ya mlingano wa nguvu, Umoja wa Ulaya unapaswa kuwa makini na kulinda vizuri manufaa yake ili usije ukageuzwa kuwa wenzo wa kufanikishia malengo ya pande mbili zinazochuana kwenye mabadiliko hayo. Amesema, mashinikizo yanazidi kuwa makubwa kwa Umoja wa Ulaya ya kuamua kuhusu ni upande upi wenye manufaa zaidi kwake kati ya pande hizo mbili.

Dunia hivi sasa inashuhudia ushindani mkubwa baina ya China na Marekani. Nguvu za Marekani zinazidi kuporomoka

 

Ameongeza kuwa, wakati nguvu za China zinazidi kuwa kubwa, uhusiano wa Umoja wa Ulaya na Beijing hautoendelea daima kuwa wa kuaminiana, ulio wazi na wa pande mbili sawa.

Vile vile amesema, ushindani baina ya Marekani na China utakuwa na taathira kubwa na utalemaza mfumo wa pande kadhaa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, katika kundi la G20, WHO na vyombo na taasisi nyinginezo za kimataifa.