Jun 03, 2020 07:36 UTC
  • Wagiriki waandamana kupinga ubaguzi wa rangi nchini Marekani

Mamia ya watu nchini Ugiriki wamefanya maandamano mbele ya ubalozi wa Marekani mjini Athens, wakilaani mauaji ya George Floyd yaliyofanywa na polisi mzungu wa nchi hiyo.

Waandamanaji wamepiga nara za kulaani ubaguzi na ukatili wa polisi wa Marekani dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika. Aidha washiriki wa maandamano hayo wamebeba picha za George Floyd pamoja na mabango yanayohimiza kutendeka haki dhidi ya muuaji. Maandamano hayo yalisimamiwa na ulinzi mkali wa maafisa usalama kwenye viunga vya ubalozi huo wa Marekani mjini Athens.

George Floyd ambaye amekuwa nembo ya mwamko wa kupinga ubaguzi nchini Marekani

Baada ya kuibuka kwa wimbi la maandamano mapya ya kulaani ubaguzi nchini Marekani, maandamano hayo pia yamefika katika nchi nyingine za dunia. Raia wa nchi za Uingereza, Canada, Denmark, Brazil na Ujerumani nao wamefanya maandamano makubwa ya kulaani ubaguzi wa rangi nchini Marekani. Jumatatu ya tarehe 25 mwezi jana, afisa mmoja wa polisi alimuua kinyama George Floyd, Mmarekani mweusi katika mji wa Minneapolis jimbo la Minnesota. Hadi sasa maandamano makubwa yanaendelea kufanyika katika miji tofauti ya Marekani kulaani ubaguzi wa rangi nchini humo.

Tags