Masanamu yanayoashiria ubaguzi yaendelea kuvunjwa Marekani na waandamanaji wenye hasira
Waandamanaji wenye hasira nchini Marekani na maeneo mengine duniani wanaendeleza mkakati wa kuangusha, kuharibu na kuondoa masanamu ya wabaguzi wa rangi.
Katika miji mbali mbali ya Marekani waandamanaji wameendelea kuvunja masanamu ikiwa ni pamoja na sanamu la Christopher Columbus, mzungu kutoka Ulaya aliyedai kuvumbua bara Amerika na sanamu la Edward Colston aliyekuwa mfanyabiashara wa watumwa, katika karne ya 17.
Waandamanaji wanaopinga ubaguzi wa rangi nchini Marekani wamebomoa, kuharibu na kuvunja vichwa vya sanamu la Christopher Columbus kuanzia miji ya Boston upande wa kaskazini hadi Miami huko kusini.
Katika tukio la hivi karibuni kabisa, sanamu la Columbus limebomolewa Alhamisi katika mji wa Camden, jimboni New Jersey. Baraza la mji huo limesema linaangalia upya nembo hizo ambazo zinaashiria ubaguzi wa rangi.
Wanasiasa mbali mbali nchini Marekani wametoa wito wa kuondolewa alama zote zinazowakilisha wakoloni na wamiliki watumwa baada ya maandamano yaliyochochewa na kifo cha George Floyd wiki tatu zilizopita.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi ametaka kuondolewa kwa masanamu makubwa 11 ya wanajeshi na maafisa wa enzi za vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Marekani mwaka 1861 hadi 1865.

Hata hivyo, Rais wa Marekani Donald Trump amekaidi pendekezo hilo na kusisitiza kwamba hatofikiria kubadilisha majina ya kambi za kijeshi ambazo zimepewa majina ya majenerali wabaguzi wa rangi na ambao waliunga mkono utumwa.
Mnamo Mei 25, afisa wa polisi katika mji wa Minneapolis jimboni Minnesota nchini Marekani alimbinya shingo kwa kutumia goti kwa dakika 9 hivi George Floyd, Mmarekani mweusi mwenye asili ya Afrika hadi akakata roho.
Mauaji hayo ya kinyama yaliibua maandamano makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa Marekani kupinga ubaguzi wa rangi huku miito ikitolewa ya kulifanyia marekebisho jeshi la polisi na kuondolewa nembo zote za ubaguzi wa rangi nchini humo.