Jul 04, 2020 07:44 UTC
  • Nchi za Amerika ya Latini zashinikiza vikwazo dhidi ya Israel

Marais wa zamani na shakhsia wengine mashuhuri wa kisiasa wa nchi za Amerika ya Latini wamekosoa vikali mpango wa utawala haramu wa Israel wa kupora eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuliunganisha na ardhi nyingine ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, viongozi hao wa zamani wa kisiasa na kijamii wa Amerika ya Latini wametoa mwito wa kuwekewa vikwazo utawala huo wa Kizayuni, kama jibu kwa hatua yake ya kutaka kupora asilimia 30 ya eneo la Ukingo wa Magharibi.

Miongoni mwa shakhsia hao wa Amerika ya Latini na Caribbean wanaopinga mpango huo wa Israel unaokiuka sheria za kimataifa ni marais wa zamani wa Brazil, Lula da Silva na Dilma Rousseff, aliyekuwa rais wa Bolivia, Evo Morales, Ernesto Samper wa Colombia, Rafael Correa wa Ecuador, Jose Mujica wa Uruguay na Fernando Lugo wa Paraguay miongoni mwa viongozi wengine.

Taarifa ya pamoja ya viongozi hao ambayo pia imesainiwa na wanamuziki mashuhuri wa Brazil, Chico Buarque na Caetano Veloso imesema, "mchakato wa upande mmoja wa uunganishaji wa eneo la Ukingo wa Magharibi ulioruhusiwa na kuungwa mkono na Marekani umefuta uwezekano wa kupatikana amani ya kudumu Palestina, kwa misingi ya sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa."

Maandamamano ya kuonyesha mshikamano na wananchi wa Palestina huko Vienna, Austria

Utawala wa Kizayuni wa Israel ulikuwa umepanga uanze kutekeleza siku ya Jumatano ya tarehe Mosi Julai mpango wake haramu wa kupora na kuunganisha asilimia 30 ya ardhi za Ufukwe wa Magharibi na ardhi zingine za Palestina unazozikalia kwa mabavu, lakini ukalazimika kuakhirisha na kusogeza mbele tarehe ya utekelezaji wake baada ya kushadidi mashinikizo ya upinzani ya Wapalestina na ya nchi mbali mbali duniani.

Mpango huo ni shemu ya mpango wa kibaguzi na uliojaa njama wa Muamla wa Karne unaopigiwa upatu na kuungwa mkono na serikali ya Rais Donald Trump wa Marekiani.

Tags