Wanasayansi nchini China wagundua mbinu inayoweza kutumiwa kuangamiza nzige
https://parstoday.ir/sw/news/world-i62893-wanasayansi_nchini_china_wagundua_mbinu_inayoweza_kutumiwa_kuangamiza_nzige
Wanasayansi nchini China wamegundua mada zenye harufu ambazo hutolewa na nzige na kusababisha wajikusanye kwenye makundi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 18, 2020 21:56 UTC
  • Wanasayansi nchini China wagundua mbinu inayoweza kutumiwa kuangamiza nzige

Wanasayansi nchini China wamegundua mada zenye harufu ambazo hutolewa na nzige na kusababisha wajikusanye kwenye makundi.

Kwa mujibu wa utafiti mpya uliochapishwa kwenye jarida la Nature, uvumbuzi huo unaweza kusaidia kuzuia nzige kujikusanya kwenye makundi makubwa na kusababisha hasara kubwa kwa mazao.

Timu ya watafiti iliyoongozwa na Taasisi ya Zoolojia iliyo chini ya Akademia ya Sayansi ya China, imegundua mada mchanganyiko zenye harufu ambazo hutolewa na nzige zinazoweza kuvutia nzigo hao porini na kuunda kundi kubwa. Kulingana na utafiti huo, mada hizo zinazojulikana kama 4-vinylanisole au 4VA, zimetambuliwa kuwa ni mkusanyiko wa pheromone ambayo inahusika na tabia ya kujikusanya nzige katika makundi makubwa.

Ugunduzi huu yumkini ukawawezesha wanasayansi kutengeneza mada ambazo zitawazuia nzige kujikusanya. Aidha kuna uwezekano wa kuunda mada zinazoweza kuwaingiza nzige katika mtego ili kuwazuia kuunda makundu makubwa makubwa.

Nzige

Nzige haribifu wa jangwani mwaka huu wamevamia maeneo makubwa ya mashariki mwa Afrika na bara Arabu na kusababisha uharibifu mkubwa katika mashamba jambo ambalo limesababisha ukosefu mkubwa wa chakula na kuhatarisha maisha ya mamilioni ya watu. Miongoni mwa nchi zilizoathiriwa vibaya na nzige ni Somalia, Kenya, Ethiopia, Uganda na Yemen.

Makadirio ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani ni kwamba kati ya Juni na Desemba mwaka huu kutakuwa na idadi kubwa ya watu wasio na uhakika wa chakula Afrika Mashariki kutokana na uvamizi wa nzige wa jangwani.