Mapigano na miripuko yaua watu 81 nchini Afghanistan
Miripuko ya mabomu na mapigano nchini Afghanistan yamesababisha makumi ya watu kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa.
Gul Islam Sial, msemaji wa mkoa wa Zabul ulioko kusini mwa nchi amesema raia watatu wameuawa huku wengine wawili akiwemo mwanamke wamejeruhiwa katika mripuko wa bomu la kutegwa kando ya barabara jana Jumamosi katika mji wa Shahjoy.
Nalo jeshi la polisi la mkoa wa Sar-e-Pul wa kaskazini mwa nchi limetangaza habari ya kuuawa raia wawili katika shambulizi la bomu la kuelekezwa kutoka mbali katikati mwa mkoa huo.
Huku hayo yakijiri, Attaullah Khogyani, msemaji wa mkoa wa Nangarhar ulioko mashariki mwa Afghanistan amesema kuwa, "kundi la Taliban usiku wa kuamkia jana lilishambulia kituo cha upekuzi cha wanamgambo wenye mfungamano na serikali ya Kabul, katika wilaya ya Khogyani na kuua wanamgambo wawili. Aidha wanachama sita wa Taliban waliuawa katika makabiliano hayo."
Wakati huo huo, Kamandi ya Jeshi la Afghanistan imesema wanachama 44 wa kundi la wapiganaji wa Taliban wakiwemo viongozi wao wanne wameuawa, huku wengine 24 wakijeruhiwa katika mapigano mapya baina yao na wanajeshi wa serikali katika mkoa wa Kunduz. Kadhalika Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan imetangaza habari ya kuuawa wanachama 24 wa Taliban katika makabiliano na vikosi vya usalama vya serikali katika mikoa ya Faryab na Nimroz .
Wadadisi wa mambo wanaamini kuwa, ukosefu wa usalama na amani; na umwagaji damu unaoendelea kushuhudiwa huko Afghanistan umetokana na uingiliaji wa kijeshi wa Marekani nchini humo. Marekani iliivamia kijeshi Afghanistan mwaka 2001 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.
Katika hatua nyingine, watu 160 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika mikoa 13 hususan ya kaskazini mwa Afghanistan.