Cuba na siasa za kindumilakuwili na za kiuadui za Marekani
(last modified Tue, 01 Sep 2020 07:05:42 GMT )
Sep 01, 2020 07:05 UTC
  • Cuba na siasa za kindumilakuwili na za kiuadui za Marekani

Kwa muda mrefu Marekani imeiwekea vikwazo na mashinikizo ya kila namna nchi ya Cuba huko Amerika ya Latini kwa visingizio mbalimbali kama vile kutochunga Havana haki za binadamu, misingi ya demokrasia na madai mengine kama hayo ambayo hayana mashiko.

Marekani inaziwekea vikwazo vya kila namna nchi mbalimbali duniani katika hali ambayo yenyewe Washington ndiye mvunjaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu. Si haki za binadamu tu, lakini pia Marekani imeshindwa hata kuheshimu mapatano ya kimataifa na imekuwa ikijitoa ovyo kwenye makubaliano mbalimbali ya kimataifa bila ya kujali matokeo yake.

Miongoni mwa nchi zilizowekewa vikwazo vya miaka mingi na Marekani ni Cuba. Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Bruno Rodríguez, amesema kuwa, msimamo wa Marekani wa kupenda kujitoa bila sababu kwenye mikataba ya kimataifa na njama zake za kuimarisha silaha zake za nyuklia ni mambo yasiyokubalika kabisa na ni hatari kwa dunia nzima hasa kwa vile kwa kujitoa kwake kwenye makubaliano hayo ya kimataifa, Marekani inatumia vibaya fursa hiyo kufanyia majaribio silaha hatari za nyuklia.

Donald Trump, rais wa Marekani

 

Ikumbukwe kuwa Cuba ni katika nchi muhimu sana katika eneo la Amerika ya Latini. Nchi hiyo kama tulivyosema imekuwa chini ya mashinikizo makubwa mno kutoka kwa Marekani kwa miaka mingi. Viongozi wa Cuba katika miongo iliyopita muda wote wamekuwa wakipigania amani, urafiki, kupambana na dhulma na kupigania uadilifu. Kutokana na misimamo yao hiyo ya kisiasa, Cuba muda wote imekuwa mpinzani wa siasa za kikoloni na kiuadui za Marekani suala ambalo limewakasirisha viongozi wa tawala za kila namna zinazoingia madarakani nchini Marekani tangu mwaka 1962. Na tangu wakati huo hadi leo hii, Cuba imekumbwa na vikwazo vya kila namna kutoka kwa Marekani. Katika kipindi cha miaka minne iliiyopita, serikali ya Trump kama ilivyojiri kwa serikali zilizopita za Marekani, imeendelea kuiwekea vikwazo Cuba, mara hii tab'ani kwa nguvu kubwa zaidi kiasi kwamba serikali ya Trump haikuguswa na hata janga la corona lililoikumbwa Cuba, bali imeendelea kuiwekea vikwazo katika sekta zote za afya na nyinginezo; Cuba na baadhi ya nchi za Amerika ya Latini. 

Ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa amegusia katika ripoti yake, taathira za siasa za kulazimisha na za kibeberu za Marekani na kutaka kuchukuliwe haraka hatua za kuondoa vikwazo ili kutoa mwanya wa kupatikana mahitaji ya lazima kama vifaa vya umma vya matibabu na kusisitiza kuwa, vikwazo ambavyo vimewekwa kwa jina la haki za binadamu, kwa hakika ndivyo vinavyosababisha vifo na vinawanyima wanadamu haki zao za kimsingi kama vile huduma za afya na chakula.

Ramani ya Cuba

 

Siasa za kiuadui za Marekani dhidi ya Cuba zinaendelea katika hali ambayo viongozi wa Havana kwa muda mrefu wamekuwa wakitilia mkazo siasa zao za kupenda amani na wanasisitiza kuwa wanaheshimu mikataba na ahadi zao katika eneo la Amerika ya Latini za mwaka 2014. Hata hivyo Marekani muda wote inazitangaza nchi zisizokubali kuburuzwa kuwa eti zinavunja haki za binadamu na eti hazipendi amani. Viongozi wa Havana wanasema kuwa, siasa za kiuadui za Marekani za kuingilia masuala ya ndani ya nchi kama Cuba, Nicaragua, Bolivia na Venezuela, zinavuruga amani na zinalenga kulidhibiti kikamilifu eneo hilo. 

Carlos Fernández Casio, mwanadiplomasia mwandamizi wa Cuba katika masuala ya Marekani anasema: Watu wanaohusika na kutunga sera huko Marekani wana misimamo ya kiuadui kuhusu eneo la Amerika ya Latini. Tunaona jinsi Wamarekani hao wanavyoangamiza njia zote za mawasiliano baina ya nchi za Amerika ya Latini.

Alaakullihaal, Marekani inaendelea na siasa zake za vikwazo vya kiwango cha juu zaidi dhidi ya nchi za Amerika ya Latini ikiwemo Cuba kwa madai tofauti kama ya eti kulinda haki za binadamu wakati ambapo kuna matukio mengi ndani ya Marekani ambayo ni mifano ya wazi kabisa ya uvunjaji wa haki za binadamu kama alivyosisitiza Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba.