Russia yakanusha madai ya Ujerumani ya kumpa sumu Navalny
-
Dmitry Peskov
Russia imekadhibisha madai kuwa Moscow ilimpa sumu mwanasiasa wa upinzani wa nchi hiyo Alexey Navalny ambaye anaendelea kupatiwa matibabu nchini Ujerumani.
Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Russia (Kremlin), Dmitry Peskov amekanusha vikali wazo lolote la kutaka kuibebesha Moscow dhima ya tukio hilo la kupewa sumu mwanasiasa huyo wa upinzani.
Amesema madai ya Ujerumani kuwa serikali ya Moscow ilihusika na jinai hiyo hayana msingi wowote, na kwamba haiingii akilini kuanza kujadili suala la vikwazo dhidi ya nchi hiyo kwa kutegemea tuhuma zisizo na mashiko.
Kremlin ilitoa msimamo huo jana Alkhamisi, ikiwa ni siku moja baada ya Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel kudai kuwa Navalny alipewa sumu hatari ya Novichok kwa nia ya kumuua. Russia inasisitiza kuwa, badala ya nchi za Magharibi kubwabwaja, zinapaswa kushinikiza kufanyika uchunguzi huru wa kuwabaini wahusika wa jinai hiyo.
Ujerumani inadai kuwa, sumu aliyopewa Navalny, ndiyo iliyotumiwa na Moscow kumuua Sergei Skripal, jasusi wa zamani wa pande mbili mwenye asili ya Russia pamoja na binti yake mnamo Machi mwaka 2018.
Balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa aliwahi kusema huko nyuma katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC kuwa, mada ya kemikali ya Novichok iliyotumiwa kumdhuru Skripal ilitengezwa kwenye maabara ya Porton Down ambayo ni kituo kikubwa kabisa cha jeshi la Uingereza kinachohusika na utafiti wa silaha za kemikali.
Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo wa Russia katika Umoja wa Mataifa, maabara hiyo iko umbali wa maili nane tu kutoka mji wa Salisbury, mahali ilipofanyika hujuma hiyo ya kumpa sumu jasusi huyo wa pande mbili pamoja na binti yake, Yulia.