Kukiri Biden kufeli siasa za Trump mbele ya Iran
Huku wakati wa kufanyika uchaguzi wa Rais wa mwezi Novemba 2020 ukizidi kukabiria nchini Marekani, wagombea wawili wa uchaguzi huo, yaani rais wa hivi sasa Donald Trump na mpinzani wake Joe Biden wa chama cha Democrats kila mmoja amekuwa akitangaza misimamo yake kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo misimamo yao kuhusu Iran na mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Katika risala yake kwa televisheni ya CNN, Joe Biden amemkosoa Donald Trump kwa sisa zake mbovu mbele ya Iran na ametangaza siasa atakazofuata yeye kuhusu Iran iwapo atachaguliwa kuwa rais wa Marekani.
Katika risala yake hiyo kwa televisheni ya CNN, Biden amesema, siasa za serikali ya Donald Trump zimefeli mbele ya Iran na kwamba rais huyo alifanya kosa na alitenda kinyume na maslahi ya Marekani kwa hatua yake ya kujitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Ameongeza kuwa, kwa hatua yake hiyo, Trump ameifanya Marekani itengwe kimataifa kiasi kwamba katika majaribio mawili ya Washington dhidi ya Iran kwenye suala la kutaka kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Tehran, Marekani imeshindwa hata kupata uungaji mkono wa waitifaki wake wa karibu kabisa kama vile nchi za Ulaya.
Biden amegusia pia mashambulio ya makombora yaliyofanywa na Iran dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Iraq na kupelekea zaidi ya wanajeshi 100 wa Marekani kupata matatizo ya ubongo akisema, baada ya mashambulio hayo, Trump alitaka kuonesha kuwa hayakuwa mashambulizi makubwa na alidharau madhara waliyopata wanajeshi wa Marekani kwa kudai kwamba wanajeshi hao walikuwa wanaumwa na kichwa tu.
Kukiri Biden kufeli siasa za Trump mbele ya Iran ni uthibitisho kwamba hata wanasiasa wakubwa kama Joe Biden huko Marekani wanatambua kwamba, licha ya kuweko madai ya mara kwa mara ya viongozi wa serikali ya Trump, hasa Mike Pompeo, waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo wanaojiliwaza kwamba siasa za kuiwekea Iran vikwazo vya kiwango cha juu zimefanikiwa, ukweli ni kuwa, wamefeli vibaya kiasi kwamba hata marafiki wao wa jadi kama nchi za Ulaya, hawaijali tena Marekani katika suala hilo. Hata Alex Vatanka, mkurugeni wa masuala ya Iran katika taasisi ya Asia Magharibi ya mjini Washington amesema, Marekani imetengwa duniani na imebaki peke yake katika suala la Iran.
Nukta nyingine katika matamshi hayo ya Biden, ni kuikosoa kwake serikali ya Trump kwa jinai yake ya kigaidi ya kumuua kidhulma Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa zamani wa Kikosi cha Quds, cha Jeshila Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH. Biden amesema, mauaji hayo yaliyofanywa na serikali ya Trump yaliifanya Iran ilipize kisasi kwa kuishambulia kwa makombora kambi ya wanajeshi wa Marekani nchini Iraq na kupelekea wanajeshi zaidi ya 100 wa Marekani kujeruhiwa vibaya na kupata matatizo makubwa ya ubongo. Kwa mtazamo wa Biden, Trump ameifedhehesha Marekani kwani majibu hayo makali ya Iran ya kuipiga kwa makombora kambi ya kijeshi ya Marekani yamewaonesha walimwengu kuwa Marekani ni dhaifu ikipata watu mashujaa.
Nukta nyingine aliyoigusia Joe Biden ni pale aliposema, kama atachaguliwa kuwa Rais wa Marekani atabadilisha siasa hizo za Trump na atarejesha muungano uliopatikana kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA wa kile alichodai ni kuizuia Iran kuwa na silaha za nyuklia. Pia amesema serikali yake itatumia njia za kidiplomasia kuamiliana na kadhia ya Iran. Ameongeza kuwa, kama Iran itarejea kutekeleza kikamilifu mapatano ya nyuklia ya JCPOA basi Washington itaichukulia hatua hiyo kuwa ni nukta ya kuanzia mazungumzo mpya. Suala jingine alilosema mgombea huyo urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democrats ni kuhakikisha atalinda usalama wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Amma lililo muhimu hapa ni kwamba katika kipindi chote hiki cha zaidi ya miaka 40, viongozi wote wa Marekani, wawe wa chama cha Democrats au Republican, wote wamekuwa na misimamo ya kiuadui dhidi ya taifa la Iran na Jamhuri ya Kiislamu. Sasa hivi Biden anasema, akichaguliwa kuwa rais wa Marekani, atarejea kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA na atatumia mapatano hayo kuibana zaidi Iran na kuilazimisha kuweka makubaliano mengine. Hata hivyo mara kwa mara Iran imekuwa ikisema kwa kusisitiza kuwa, imeingia kwenye mapatano ya nyuklia kwa sababu yana faida kwake, na makubaliano hayo yanahusiana na kadhia ya nyuklia tu, si kitu kingine. Aidha inasisitiza kwamba kamwe haiwezi kusalimu amri mbele ya mashinikizo ya yeyote yule, si Marekani pekee na masuala kama nguvu zake za makombora ni mambo ambayo hayamo kabisa katika mjadala.