Urusi yaikosoa Ujerumani kwa kukataa kuipatia rekodi za matibabu za Navalny
-
Maria Zakharova
Serikali ya Russia imeikosoa Ujerumani kwa kukataa kuipatia Moscow maelezo ya kimatibabu ya mpinzaji wa Russia, Alexei Navalny ambaye Magharibi inadai amepewa sumu, na badala yake imeipeleka kesi hiyo kwenye Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW).
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova amesema kuwa analaimika kusema kwamba hii ni njia ya kukimbia na kukwepa uhakika. Zakharova amesema: Kama madai kwamba Russia ndiyo iliyompa sumu Alexei Navalny ni ya kweli basi wekeni wazi na tupeni uhakika huo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema kuwa inasikitisha kuona kuwa mwenendo huu haukomi na kumalizika.
Alexey Navalny alipatwa na matatizo ya kiafya tarehe 20 mwezi uliopita wa Agosti akiwa kwenye ndege iliyokuwa ikielekea Moscow kutoka mji wa Tomsk huko Siberia na akalazwa hospitalini. Baadaye alipelekwa Ujerumani kwa ombi la serikali ya nchi hiyo.
Ujerumani inadai kuwa, sumu aliyopewa Navalny ndiyo iliyotumiwa na Moscow kumuua Sergei Skripal, jasusi wa zamani wa pande mbili mwenye asili ya Russia pamoja na binti yake mnamo Machi mwaka 2018.
Hata hivyo balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa aliwahi kusema huko nyuma katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC kuwa, mada ya kemikali ya Novichok iliyotumiwa kumdhuru Skripal ilitengezwa kwenye maabara ya Porton Down ambayo ni kituo kikubwa kabisa cha jeshi la Uingereza kinachohusika na utafiti wa silaha za kemikali.
Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo wa Russia katika Umoja wa Mataifa, maabara hiyo iko umbali wa maili nane tu kutoka mji wa Salisbury, mahali ilipofanyika hujuma hiyo ya kumpa sumu jasusi huyo wa pande mbili pamoja na binti yake, Yulia.