Newsweek: Serikali ya Trump inaficha ugaidi wa ndani unaofanywa na wazungu
(last modified Fri, 25 Sep 2020 08:23:45 GMT )
Sep 25, 2020 08:23 UTC
  • Newsweek: Serikali ya Trump inaficha ugaidi wa ndani unaofanywa na wazungu

Jarida la kila wiki la Newsweek nchini Marekani limechapisha makala ya mshauri wa zamani wa Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo (Pentagon) Jasmine el Gamal ambaye amesema kuwa licha ya kupita mwaka mmoja sasa tangu Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani iliyoanzishwa baada ya mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 kutangaza azma yake ya kupambana na ugaidi wa ndani na vitisho vya wazungu wenye misimamo mikali, lakini uchunguzi unaonesha kuwa, wizara hiyo haijachukua hatua yoyote katika uwanja huo.

Jasmine el Gamal amesema kuwa Rais Donald Trump amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kuchochea misimamo mikali na kwa msingi huo ukatili na ugaidi wa ndani wa wazungu utaendelea kuwepo bila ya kupatiwa dawa maadamu kiongozi huyo atakuwepo madarakani.

Makala ya Jasmine el Gamal imeashiria uchunguzi uliofanywa na taasisi ya kutetea haki za kiraia ya Anti-Defamation League unaoonyesha kwamba asilimia 90 ya operesheni za mauaji yaliyotokana na misimamo mikali nchini Marekani mwaka 2019 zilihusishwa na makundi ya wazungu wenye misimamo mikali.

Hivi karibuni Mkurugenzi wa Idara ya Upelezi ya Marekani (FBI) aliiambia Kamati ya Mahakama ya Kongresi ya nchi hiyo kwamba, wazungu wenye misimamo mikali wanaohusika na ukatili kwa sababu za kibaguzi au kimbari wanaunda sehemu kubwa zaidi ya uchushunguzi wa FBI kuhusiana na ugaidi.

Christopher Asher Wray alisisitiza kuwa hujuma nyingi za wafuasi wa makundi hayo zinatokana na itikadi kwamba wazungu na watu weupe ndio kizazi bora zaidi.