Macron: Uturuki imetuma mamluki wa Kisyria kupigana Nagorno-Karabakh
Ufaransa imeituhumu Uturuki kwamba imetuma mamluki wa Kisyria kupigana vita katika mzozo wa Nagorno-Karabakh na kusema Paris inashirikiana na Russia kwa ajili ya kusitisha mapigano kati ya majeshi ya Azerbaijan na Armenia.
Hayo yamesemwa katika taarifa iliyotolewa na ofisi ya Rais wa Ufaransa, Emmanue Macron Alkhamisi ya leo. Hata hivyo Rais wa Ufaransa hakutoa ushahidi wowote wa kutia nguvu madai kwamba Uturuki imetuma mamluki wa Kisyria kupigana katika eneo la Nagorno-Karabakh kwa maslahi ya Azerbaijan.
Macron, ambaye amekuwa kwenye vita vya maneno na Rais wa Uturuki, Tayyip Erdogan kwa miezi kadhaa, alisema jana Jumatano kwamba "Ankara imeamua kuwa na mienendo ya kivita".
Jumatatu iliyopita balozi wa Armenia mjini Moscow alisema kuwa Uturuki imetuma karibu wapiganaji 4,000 kutoka kaskazini mwa Syria kwenda Azerbaijan kwa ajili ya kushiriki katika mapigano. Madai hayo yamepingwa na msaidizi wa Rais wa Azabajani, Ilham Aliyev na serikali ya Uturuki.

Kwa upande wake Russia imetahadharisha kuhusu hatua ya kutumia mamluki wa kigeni katika mapigano ya eneo la Nagorno-Karabakh na kuwataka viongozi wa nchi zinazoshiriki katika mapigano hayo kuzuia hatua yoyote ya kutumia magaidi na mamluki wa kigeni katika mapigano hayo. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Rusia imetahadharisha kuwa kupelekwa mamluki wa kigeni katika vita vya Nagorno-Karabakh kutakuwa tishio la muda mrefu kwa kanda nzima ya Kaukasi.
Vita kati ya majeshi ya nchi za Azerbaijan na Armenia vinaendelea kwa siku kadhaa sasa katika eneo hilo linalogombaniwa, na kila upande unadai kusababisha hasara kubwa kwa upande mwingine.