Washington Post: Kuwakandamiza wapigakura weusi kunairejesha Marekani karne ya 19
(last modified Mon, 19 Oct 2020 15:40:07 GMT )
Oct 19, 2020 15:40 UTC
  • Washington Post: Kuwakandamiza wapigakura weusi kunairejesha Marekani karne ya 19

Gazeti la Washington Post la Marekani limechapisha makala inayokituhumu chama tawala cha Republican kinachoongozwa na Donald Trump kuwa kinawakandamiza wapigakura weusi na kwamba kina malengo sawa na yale ya makundi ya wabaguzi wa rangi yanayoamini kuwa watu weupe ndio kizazi bora zaidi kuliko watu wa rangi nyingine.

Gazeti hilo limeandika kuwa, chama cha Republican kinatekeleza siasa za kibaguzi kama zile zilizokuwa zikitekelezwa na serikali za majimbo ya Kusini mwa Marekani katika kipindi cha karne ya 19 ambazo ziliwanyima raia weusi wenye asili ya Afrika haki ya kupiga kura.

Washington Post imesema kuwa, ukandamizaji wa wapigakura weusi nchini Marekani unairejesha nchi hiyo katika kipindi cha karne ya 19 na kwamba, hakuna tofauti baina ya malengo ya chama cha Republican kinachoongozwa na Donald Trump na kundi la Ku Klux Klan; kwa sababu vyama hivyo viwili vinafanya jitihada za kutatiza upigaji kura wa Wamarekani weusi. 
Washington Post imeripoti kuwa, kama yalivyokuwa yakifanya makundi ya wabaguzi wa rangi katika karne ya 19 katika majimbo ya Kusini mwa Marekani, hii leo chama cha Republican na waungaji mkono wa Trump wanalenga maeneo yenye idadi kubwa ya wapigakura weusi na jamii za waliowachache. 

Wamarekani weusi wakipigania haki ya kupiga kura katika karne ya 19

Makala ya Washington Post imesema: "Marekani ya Trump inaishi katika karne ya 19, lakini tunapaswa kujifunza kutokana na tajiriba ya kipindi cha miaka 150 iliyopita." 

Uchaguzi wa rais wa Marekani umepangwa kufanyika tarehe 3 mwezi ujao wa Novemba, na kura za maoni zinaonyesha kuwa mgombea wa chama cha Democratic, Joe Biden, anamtangulia Donald Trump anayebeba bendera ya chama cha Republican katika kinyang'anyio hicho.