Nov 07, 2020 10:14 UTC
  • Uchaguzi wa rais wa 2020; nembo ya demokrasia bandia ya Marekani

Kama ilivyokuwa imetabiriwa awali, uchaguzi wa mwaka huu wa rais wa Marekani ambao ulifanyika tarehe 3 mwezi huu wa Novemba umekuwa moja ya chaguzi zenye utata mkubwa zaidi katika historia ya nchi hiyo, uchaguzi ambao taathriza zake bila shaka zitabakia kwa muda mrefu katika uwanja wa siasa za nchi hiyo.

Hivi sasa demokrasia ambayo Marekani imekuwa ikiihubiri na kuipigia debe kwa miaka mingi duniani inatiliwa shaka na jamii ya kimataifa. Akizungumzia suala hilo na kuashiria kucheleweshwa kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni na vilevile madai ya Rais Donald Trump wa Marekani kwamba udanganyifu mkubwa umefanyika katika uchaguzi huo, Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amesema kuwa ni kichekesho kwamba Marekani imekuwa ikijaribu kuwafundisha Wavenezuela somo la demokrasia. Amekosoa ucheleweshaji wa kuhesabiwa kura huko Marekani na kusisitiza kuwa kinyume na ilivyo nchi hiyo ya Magharibi, Venezuela ina mfumo madhubuti na wa wazi wa kuhesabu kura.

Maduro ameashiria mkondo wa uchaguzi wa rais huko Marekani na kusema kuwa kinyume na inavyoshuhudiwa nchini humo, katika nchi yake ya Venezuela, matokeo ya uchaguzi hujulikana usiku wa siku ya kupigwa kura na kutangazwa kwa njia ya wazi kabisa. Marekani inadai kwamba serikali ya Maduro imeharibu demokrasia huko Venezuela na kwa hivyo inapasa kuondoka madarakani.

Maduro anaashiria mkondo wa uchaguzi wa rais wa Marekani ambapo licha ya kuwa una utata mwingi, sasa umeibua tuhuma za Trump dhidi ya mpinzani wake mkuu wa chama cha Demokrat, Joe Biden, ambaye licha ya takwimu kuonyesha kwamba ameshinda uchaguzi, lakini Trump amekataa kukubali kushindwa na hivyo ameamua kuibua tuhuma na uchochezi dhidi ya mfumo mzima wa kisiasa wa Marekani na kusema kuwa ni mfumo mbovu ambao umemuibia kura.

Trump anadai kuibiwa kura

Licha ya siku nne kupita tokea kufanyika uchaguzi, na kura za walioshiriki zoezi hilo kwa njia ya posta zikiendelea kuhesabiwa, lakini Trump ameamua kuendesha vita dhidi ya mfumo wa uchaguzi wa nchi yake na kuendelea kutoa madai ya kuibiwa kura. Akizungumza mbele ya waandishi siku ya al-Khamisi, Trump alisema mfumo wa uchaguzi wa nchi hiyo ni mbovu na kwamba umehusika katika kumuibia kura.

Swali muhimu linalopaswa kuulizwa hapa ni kwamba je, ni kwa nini aliposhinda uchaguzi wa mwaka 2016 kwa kutumia mfumo huo huo wa upigaji kura alikubali matokeo yake bila kusita na wala hakuchukua hatua yoyote ya kuukosoa, lakini sasa ambapo anaona kuwa ameshindwa ameamua kuupiga vita na kutilia shaka itibari yake?

Kwa mujibu wa Michael Georg, Mkuu wa Taasisi ya Usalama na Ushirikiano Barani Ulaya, OSCE, tuhuma ambazo Trump anazitoa dhidi ya wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo tofauti ya Marekani ni sawa na kutilia shaka demokrasia. Anasisitiza kwa kusema, ni wazi kuwa Trump anatumia vibaya madaraka yake ya rais wa Marekani.

Suala jingine ni kuwa, Trump akiwa rais wa Marekani anadhibiti vyombo na taasisi zote zilizo chini ya serikali kuu ya nchi hiyo na hivyo ni jambo la kuchekesha kuwa anadai kufanyika mizengwe na udanganyifu katika upigaji kura katika hali ambayo kwa kawaida ni mpinzani wake Jeo Biden, ndiye anapasa kutoa madai kama hayo.

Swali jingine linaloulizwa na wengi ni kuwa je, demokrasia ambayo Marekani siku zote imekuwa ikiipigia makelele na kuzivamia nchi nyingine duniani, zikiwemo Afghanistan na Iraq, kwa madai ya kuitetea, ndiyo hiyo hiyo inayotekelezwa hivi sasa huko Marekani au ni demokrasia tofauti?

Magenge ya kibaguzi yanayotumiwa na Trump dhidi ya wapinzani wake

Bila shaka moja ya misingi muhimu ya demokrasia ni kushirikishwa wananchi katika kuwachagua viongozi wao. Leo Trump si tu kwamba anadai kuwa mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo ni mbovu, bali kimsingi anatilia shaka mfumo mzima wa uchaguzi. Kwa kusisitiza kwamba kura zake nyingi zimeibwa, ni wazi kuwa anatilia shaka mwenendo wa hivi sasa wa uchaguzi wa Marekani ambao pia ulipelekea kuchaguliwa kwake na kumuingiza White House mwaka 2016.

Ikiwa kweli Trump ameibiwa kura kirahisi hivyo kupitia mfumo wa upigaji kura wa Marekani basi ni wazi kuwa msingi wa demokrasia wa nchi hiyo umeoza na unapasa kufanyiwa marekebisho ya msingi.

Jamii ya Marekani hii leo imegawanyika katika makundi mawili ambapo kuna hatari ya kutokea ghasia ambazo zinaweza kuibua mapigano ya silaha ya wenyewe kwa wenyewe kati ya wafuasi wa wagombea wawili wakuu wa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo, kama tunavyoona kuwa tayari dalili za ghasia hizo zimeanza kudhihiri katika baadhi ya sehemu za nchi hiyo.

 

Tags