Takwa la harakati ya Black Lives Matter kwa Joe Biden
Ukatili mkubwa na ubaguzi wa rangi wa kimfumo dhidi ya watu weusi daima vimekuwa miongoni mwa sifa kuu za jamii ya Mareikani tangu nchi hiyo ilipoasisiwa. Wamarekani weusi wamekuwa wakikumbana na sulubu na mashaka mengi ya aina mbalimbali za ubaguzi na ukatili licha ya miaka mingi ya mapambano ya kupigania haki zao.
Sasa na baada ya Joe Biden kuibuka mshindi katika uchaguzi wa rais wa Marekani, raia weusi wa nchi hiyo wamemtaka mwanasiasa huyo kuchukua hatua madhubuti za kukomesha manyanyaso, ukatili na ubaguzi wanaokumbana nao katika jamii ya Marekani.
Harakati ya Black Lives Matter imemwandikia barua rais mteule wa Marekani, Joe Biden na makamu wake Kamala Harris ikiwataka wayape kipaumbele matakwa ya Wamarekani weusi.
Katika barua hiyo, harakati Black Lives Matter inayopinga ubaguzi wa rangi imeomba kukutana na kufanya mazungumzo na Joe Biden na makamu wake, Kamala Harris na kusisitiza kuwa, kuondoka Donald Trump katika ikulu ya White House si dhamana ya kukomeshwa hali mbaya na isiyovumilika ya Wamarekani weusi.
Harakati hiyo imesema kuwa: "Wamarekani weusi ndio walioshinda uchaguzi na wanataka sauti yao isikike na matakwa yao yapewe kipaumbele, si kwa sababu tu Wamarekani weusi ni wapiga kura waaminifu wa chama cha Democtaric bali pia kwa sababu wanaishi katika hali mbaya katika nchi iliyoasisiwa kwa misingi ya kibeberu."

Barua muhimu ya harakati ya Black Lives Matter kwa Joe Biden kwa hakika inaonyesha matakwa ya Wamarekani weusi ambao wanaunda asilimia karibu 12 ya jamii yote ya Marekani ikimtaka afanye jitihada kubwa za kutekeleza ahadi zake alizotoa kwenye kampeni za uchaguzi wa rais kuhusiana na kukomesha tatizo la ubaguzi wa rangi na kupunguza ukatili wa polisi ya Marekani dhidi ya jamii yao. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, katika hotuba yake aliyotoa tarehe 7 mwezi huu wa Novemba baada ya ushindi, Joe Biden aliahidi kung'oa mizizi ya ubaguzi wa rangi wa kimfumo nchini Marekani. Katika kampeni zake za chaguzi mwezi Juni mwaka huu, Biden alikiri katika ukurasa wake wa Twitter kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa Marekani kwamba ubaguzi wa rangi wa kimfumo nchini Marekani una historia ya zaidi ya karne mbili. Biden aliandika katika ujumbe huo kwamba: "Ubaguzi wa rangi wa kimfumo una umri wa zaidi ya miaka 200 nchini Marekani na unaendelea kuwa na taathira haribifu katika jamii ya nchi hii."
Marekani kamwe haikufuata misingi wa kuasisiwa kwake, yaani " wananchi wote wako sawa katika maumbile", na msingi huu unaendelea kupuuzwa hadi hii leo. Hii ina maana kwamba, rais mteule wa Marekani mwenyewe anaelewa vyema dhulma na manyanyaso yanayoendelea kuwakumba Wamarekani weusi kwa karne kadhaa sasa.
Hata hivyo inatupasa kukiri kwamba, kutokana na ubaguzi hususan ubaguzi wa rangi wa kimfumo kukita mizizi katika jamii ya Marekani na msimamo wa asasi na taasisi nyingi za nchi hiyo wa kutaka kudumishwa mfumo huo, hakuna matumaini ya kufanyika mabadiliko ya kimsingi kwa maslahi ya Wamarekani weusi au kukomeshwa kabisa ubaguzi na ukatili wa vyombo vya usalama dhidi ya jamii ya watu hao.

Hata hivyo kukiri Biden kwamba Wamarekani weusi wanasumbuliwa na hali mbaya na ubaguzi wa rangi wa kimfumo katika nchi ya Marekani inayojinadi kuwa kinara wa haki za binadamu duniani, kunafichua tena hali halisi na ukweli mchungu wa jamii ya nchi hiyo.
Kwa hakika ubaguzi wa rangi, ubaguzi katika sekta ya elimu, masuala ya jamii, ajira na ukatili wa vyombo vya dola hususan polisi na askari usalama dhidi ya Wamarekani weusi limekuwa jambo la kawaida nchini Marekani. Licha ya kwamba harakati ya kupigania haki za kiraia za watu weusi iliibua wimbi kubwa nchini Marekani katika muongo wa 1950 katika kupigania haki za jamii hiyo na kupinga ubaguzi, lakini hali ya sasa ya jamii ya nchi hiyo inaakisi kuendelea kuwepo ubaguzi wa rangi wa kimfumo katika ngazi na sekta zote.
Katika uwanja huu rais wa zamani wa Marekani Barack Obama anasema: Ubaguzi wa rangi umo katika vinasaba (DNA) vya Wamarekani.
Miongoni mwa vielelezo vya uovu huo uliokithiri katika miaka ya karibuni ni ukatili uliopindukia wa polisi ya Marekani dhidi ya raia weusi. Takwimu zinaonyesha kuwa, raia wasio wazungu hususan wale wenye asili ya Afrika ndio wahanga wakuu wa ukatili wa polisi ya Marekani na suala hii ni miongoni mwa sababu za maandamano na machafuko yanayoibuka mara kwa mara katika miji mbalimbali ya Marekani. Chanzo na mzizi wa haya yote ni ubaguzi wa rangi wa kimfumo uliokita mizizi baina ya Wamarekani.

Kuendelea ukatili na ubaguzi huo kumesababisha maafa ya kutisha kama yale ya mauaji ya George Floyd aliyeuliwa kwa kubinywa shingo na polisi mzungu tena kwa damu baridi kabisa na kadamnasi. Van Jones mtangazaji na mchambuzi wa televisheni ya CNN ya Marekani anaashiria mauaji ya kusikitisha ya George Floyd na kusema: "Si George Floyd peke yake aliyebinywa shingo na kushindwa kupumua, bali kwa hakika kuna Wamarekani wengi ambao wanahisi kukabwa shingo na wanashindwa kupumua."