Watu kadhaa watiwa mbaroni Ujerumani kwa kupanga njama za kuwashambulia Waislamu
Maafisa wa mahakama nchini Ujerumani wametangaza kuwa, watu kadhaa wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kupanga mashambulio dhidi ya Waislamu na misikiti katika nchi hiyo ya bara Ulaya.
Kanali ya Televisheni ya al-Alam imewanukuu maafisa wa mahakama wa Ujerumani wakitangaza kuwa, watu 12 wametiwa mbaroni wakituhumiwa kupanga njama za kushambulia misikiti na kuwaua Waislamu.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, lengo la njama hizo ni kuanzisha vita vya ndani. Kwa mujibu wa vyombo vya mahakama nchini Ujerumani ni kuwa, 11 kati ya waliotiwa mbaroni ni wanachama wa genge moja huku aliyebakia yeye alikuwa akishirikiana tu na kundi hilo na kwamba, wote ni raia wa Ujerumani.
Mwenendesha mmoja wa Ujerumani ameziambia duru za habari kwamba, watuhumiwa hao walikuwa wakikutana mara kwa mara na waliahidi kutoa fedha za kununua silaha.
Mwanachama mwingine wa genge hilo aliyefanikiwa kutoroka wakati wa operesheni ya kuwatia mbaroni anaendelea kusakwa na vyombo vya usalama vya Ujerumani.

Nchini Ujerumani kikawaida mashambulio na hujuma dhidi ya Waislamu na maeneo yao ya ibada hufanywa na makundi ya mrengo wa kulia yenye misimamo ya kufurutu ada.
Vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu vimeongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni katika ulimwengu wa Magharibi.
Hata hivyo licha ya propaganda chafu dhidi ya Uislamu, raia wa Magharibi wanaosilimu na kuingia katika Uislamu imekuwa ikiongezeka siku baada ya siku na Uislamu unatajwa kuwa dini inayokuwa kwa kasi barani Ulaya.