Rais wa Afghanistan: Mazungumzo ya amani yamefikia hatua nyeti na hasasi
Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan amesema, awamu iliyofikiwa hivi sasa katika mazungumzo ya kutafuta suluhu na kurejesha amani nchini humo kati ya serikali na kundi la Taliban ni hasasi na muhimu sana.
Ashraf Ghani ameyasema hayo mjini Kabul katika hafla ya uzinduzi wa kamati ya uongozi na wajumbe wa Baraza Kuu la Maslahi ya Taifa la nchi hiyo.
Sambamba na kusisitiza kuwa kurejeshwa amani nchini humo ndilo takwa kuu la Waafghani wote, Rais Ashraf Ghani amesema, baada ya mchakato wa mazungumzo ya amani kuivuka awamu ya kwanza, hivi sasa umefika kwenye awamu ya pili ambayo ina umuhimu na unyeti mkubwa sana.
Rais wa Afghanistan amebainisha kuwa, ujumbe wa serikali katika mazungumzo ya amani na kundi la Taliban umetetea na kuunga mkono mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, katiba na maazimio ya Baraza Kuu la Ushauri juu ya amani la Loya jirga.
Baraza Kuu la Maslahi ya Taifa la Afghanistan liliundwa miezi takriban sita iliyopita baada ya mwafaka wa kisiasa uliofikiwa kati ya Ashraf Ghani na Abdullah Abdullah, ambaye ndiye mkuu wa baraza hilo; na kikao chake cha kwanza kilifanyika jana.
Mazungumzo ya amani ya Afghanistan kati ya serikali na kundi la Taliban yalianza tarehe 12 Septemba katika mji mkuu wa Qatar, Doha; na ajenda za awamu ya mwisho ya mazungumzo hayo zilikamilishwa siku chache zilizopita na hivi sasa pande hizo zinajadiliana juu ya namna ya kutatua tofauti zilizopo baina yao.
Wananchi wa Afghanistan wana matumaini kwamba kupiga hatua mazungumzo hayo kutahitimisha vita na mauaji nchini mwao ili waweze kurejea kwenye maisha yao ya kawaida.../