NAM yalaani hatua ya Marekani kupora mali za Iran
Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) imelaani hatua ya Marekani ya kupora mali za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Harakati hiyo yenye nchi wanachama 120 imetoa taarifa maalumu na kueleza kwamba hatua hiyo ya Marekani ya kuidhinisha kuchukuliwa mali za Iran zilizozuiwa nchini humo ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.
Taarifa ya NAM imefafanua kuwa uamuzi uliochukuliwa na Washington ni ukiukaji wa mikataba na majukumu ya kimataifa kuhusiana na "kinga ya kujitawala ya mataifa".
Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote aidha imetahadharisha kupitia taarifa yake hiyo kuwa kushindwa Washington kuheshimu msingi huo kutakuwa na taathira mbaya ikiwemo "kuvuruga uthabiti na kusababisha mchafukoge katika mahusiano ya kimataifa."
NAM imeikosoa Kongresi ya Marekani kwa kufungua njia kwa utaifishaji haramu wa mali za kigeni na hatua ya serikali ya nchi hiyo ya kuzuia mali hizo.
Mahakama Kuu ya Marekani ilitoa uamuzi Aprili 20 kwamba mali za Iran zenye thamani ya dola bilioni mbili ambazo zinazuiwa kwenye akaunti ya benki nchini humo zigawanywe kwa familia za Wamarekani waliouliwa katika shambulio la bomu lililotokea mwaka 1983 mjini Beirut, Lebanon pamoja na mashambulio mengine ambayo Marekani inayahusisha na Iran. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha kuhusika na mashambulio yote hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Muhammad Javad Zarif amekitaja kitendo cha kuchukuliwa mali hizo za Tehran zinazozuiliwa Marekani kuwa ni "uharamia" na kusisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itahakikisha mali hizo zinarejeshwa kwa namna yoyote ile.../