Madaktari wanne na mpita njia wauawa katika hujuma ya kigaidi Afghanistan
Madaktari wanne na mpita njia wameuawa Jumanne katika hujuma ya kigaidi katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.
Taarifa zinasema madaktari hao wanne walikuwa wanafanya kazi katika gereza Pul-e-Charkhi yenye mamia ya wafungwa wa kundi la wanamgambo wa Taliban.
Msemaji wa polisi katika mji mkuu Kabul, Ferdaws Faramarz, amethibitisha kuwa mripuko huo umetokea katika wilaya ya kusini mwa mji huo wakati madaktari hao walipokuwa wakisafiri kuelekea katika gereza hilo walimokuwa wakifanya kazi.
Mamia ya wapiganaji wa Taliban na wahalifu wengine wamefungwa katika gereza la Pul-e-Charkhi, lililoko katika viunga vya mji wa Kabul. Mji huo umekumbwa na wimbi la ghasia katika miezi ya hivi karibuni licha ya kundi la Taliban na serikali kushiriki mazungumzo ya amani. Hadi sasa hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na hujuma hiyo.
Milipuko ya kigaidi imeongezeka miezi ya hivi karibuni nchini Afghanistan pamoja na kuwa mazungumzo baina ya wanamgambo wa Taliban na serikali ya Afghanistan yamekuwa yakifanyika nchini Qatar.

Hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulionya kuhusu ongezeko la mashambulizi dhidi ya raia na kutozingatiwa sheria za kibinadamu nchini Afghanistan.
Kundi la kigaidi la ISIS nalo limedai kuhusika na hujuma kadhaa dhidi ya maeneo ya raia ikiwemo misikiti nchini Afghanistan.
Marekani iliongoza waitifaki wake katika hujuma ya kijeshi Afghanistan Oktoba 2001 kwa kisingizio cha kukabiliana na ugaidi. Hatahivyo ugaidi umeongezeka nchini humo na hadi sasa usalama haujaweza kupatikana. Uzalishaji wa dawa za kulevya nchini humo umeongezeka kwa kiasi kikubwa. Katika mwaka 2000 na 2001, ukulima wa mihadarati Afghanistan ulikuwa ni tani 200 lakini baada ya askari wa Marekani kuvamia nchi hiyo, kiwango hicho kimeongezeka na kufika takribani tani 10,000.