Guterres : COVID-19 imetufunza hatuwezi kupuuza hatari, ataka chanjo igaiwe kiuadilifu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema kuwa maambukizi ya kirusi cha corona na kuenea ugonjwa wa COVID-19 pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa, ni changamoto mbili kuu ulizoikumbwa dunia hivi sasa.
Aidha amekiri kwamba hakuna uadilifu katika ugawaji wa chanjo ya corona kati ya nchi tajiri na maskini, kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea na ametaka kufanyike uadilifu katika ugawaji wa chanjo za corona.
Amesema hayo kwa njia ya video katika hotuba yake kwenye mkutano wa kimataifa wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ulioandaliwa nchini Uholanzi. Mkutano huo unaofanyikwa kwa njia ya Intaneti ulianza jana Jumatatu Januari 25 na unamalizika leo Jumanne. Guterres amesema, mwaka huu umeanza kwa kumbusho la umuhimu wa kukabili kwa nguvu zaidi na changamoto zinazoikabili dunia.
Amesema “changamoto ya tabianchi ni hatari ambayo sote tunaitambua. Sayansi imeweka bayana kwamba tunakabiliwa na dharura ya mabadiliko ya tabianchi. Tayari tunashuhudia matukio yasiyo ya kawaida ya mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yanaathiri maisha na uwezo wa watu kuishi katika mabara yote.”
Ameongeza kuwa, hali hii haiwezi kupuuzwa tena kwani kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO, kumekuwa na majanga zaidi ya 11,000 ambayo yametokana na hali ya hewa, mabadiliko ya tabianchi na maji katika miaka 50 iliyopita na kuigharimu dunia takribani dola trilioni 3.6. Majanga hayo pia yamepoteza maisha ya zaidi ya watu 410,000 katika muongo mmoja uliopita wengi wao wakiwa ni kutoka katika nchi za kipato cha chini na cha kati.