Marekani yakataa kuondoa kikamilifu wanajeshi wake walioko Afghanistan
Marekani imetazama upya aghalabu ya sera na hatua za serikali iliyotangulia ya Trump baada ya kuingia madarakani serikali mpya ya Joe Biden. Siasa za Washington kuhusu Afghanistan na kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini humo ni kati ya masuala hayo.
John Kirby Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) Alhamisi iliyopita alidai kuwa kundi la Taliban halijaheshimu ahadi yake kwa mujibu wa makubaliano iliyofikia na Marekani, na kwa sababu hiyo Washington haitaweza kuondoa kikamilifu wanajeshi wake huko Afghanistan kufikia mwezi Mei mwaka huu. Amedai kuwa Marekani itaendelea eti kufungamana na ahadi zake za kutatua hitilafu katika mazungumzo. Matamshi ya afisa huyo wa Pentagon yametolewa baada ya Antony Blinken Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kusisitiza katika mazungumzo ya simu na Rais Ashraf-Ghani wa Afghanistan kuwa serikali ya Biden inaunga mkono mazungumzo ya amani ya nchi hiyo.
Makubaliano baina ya Marekani na Taliban yalisainiwa mwezi Februari mwaka jana huko Doha Qatar wakati wa utawala wa Trump. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, ilitazamiwa kuwa wanajeshi wote wa Marekani wangeondolewa huko Afghanistan kufikia Mei mwaka huu iwapo kundi la Taliban lingetekeleza ahadi zake. Aidha ilitazamiwa kuwa mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Afghanistan na Taliban yangeanza hata hivyo sehemu hiyo ya makubaliano pia haijazaa matunda. Pamoja na hayo, masuala mawili yameibua utata na shaka kuhusu utekelezaji wa makubaliano hayo.
Sababu ya kwanza ni kuwa, serikali ya Biden haiafiki suala la kuondolewa kikamilifu wanajeshi wa Marekani huko Afghanistan sawa kabisa na kama yalivyo maamuzi mengine mengi yaliyochukuliwa na serikali ya Trump.
Viongozi wa serikali ya Biden kama Jake Sullivan, Mshauri wa Usalama wa Taifa na Antony Blinken Waziri wa Mashauri wa nchi hiyo hivi karibuni wamesisitiza juu ya kuangaliwa upya makubaliano yaliyofikiwa kati ya serikali ya Trump na kundi la Taliban. Serikali ya Afghanistan na Taliban huko nyuma zilieleza kuwa, pande mbili zinasubiri Biden aingie White House ili kusogeza mbele makubaliano hayo ya Doha na kufahamu misimamo na maamuzi yake kuhusu makubaliano hayo. Taliban imetahadharisha kuwa, italazimika kuchukua maamuzi magumu iwapo Marekani haitafungamana na ahadi yake ya kuwaondoa kikamilifu wanajeshi wake huko Afghanistan. Baada ya kusainiwa makubaliano kati ya Marekani na Taliban mwezi Februari mwaka jana huko Doha Qatar; kwa mujibu wa amri ya Trump, wanajeshi wa Marekani walioko Afghanistan wamepunguzwa kutoka 4500 na kufikia 2500 hadi kufikia katikati ya mwezi Januari mwaka huu. Aidha kwa mujibu wa makubaliano hayo, wafungwa elfu tano wa kundi la wanamgambo wa Taliban pia wameachiwa huru kutoka katika jela za serikali ya Afghanistan; ambapo sasa serikali hiyo imetangaza kuwa wafungwa wengi miongoni mwao wamerejea katika medani ya vita.
Sababu ya pili ambayo imekuwa kisingizio kwa Marekani cha kuendela kubakisha wanajeshi wake huko Afghanistan ni kuendelea mashambulizi ya silaha na ya kujitoa mhanga ya Taliban dhidi ya maeneo ya vikosi vya usalama na askari jeshi na pia katika miji mbalimbali ya nchi hiyo. Taliban iliahidi kuacha kuibua machafuko na kuanza mazungumzo na serikali kuu ya Afghanistan ili kurejesha amani nchini humo. Ni wazi kuwa, Taliban inatumia fursa hiyo kushadidisha mashambulio yake dhidi ya vikosi vya serikali.
Hamdullah Mohib Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Afghanistan ametahadharisha kuwa nchi hiyo inakabiliwa na tishio kuu la vita vya ndani baada ya Marekani kujiandaa kuondoka Afghanistan. Marekani katika miaka ya mwisho ya utawala wa Trump imesababisha ombwe la kiusalama huko Afghanistan kwa hatua yake ya kuondoka nchini humo bila mpangilio maalumu. Kongresi ya Marekani na Pentagon haziafiki kuondolewa wanajeshi wote wa Marekani huko Afghanistan, na kwa hiyo mabadiliko ya kimsingi yalitazamiwa kujiri katika sera za Washington kuhusiana na Afghanistan baada ya kuingia madarakani serikali mpya huko White House; jambo ambalo kidhahiri linaonekana kufikiwa baada ya Pentagon kutangaza msimamo wake kwamba wanajeshi wa Marekani hawataondoka kikamilifu huko Afghanistan.