Iran itatoa jibu kali kwa tishio na uchokozi wowote wa Israel
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ametahadharisha juu ya matamshi ya kichokozi na ya kupiga ngoma ya vita ya maafisa wa utawala haramu wa Israel na kusema kuwa, Tehran itatoa jibu kali kwa tishio lolote la Wazayuni dhidi yake.
Majid Takht Ravanchi amesema hayo katika barua yake kwa Katibu Mkuu wa Umoja na Mataifa, Antonio Guterres na Rais wa sasa wa Baraza la Usalama la umoja huo.
Ameeleza bayana kuwa, katika siku za hivi karibuni, utawala wa Kizayuni si tu umeshadidisha matamshi ya kichochezi na kichokozi dhidi ya Iran, bali unapanga njama za kutekeleza hatua za kiuhasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Takh Ravanchi ameashiria madai yasiyo na msingi yaliyotolewa Januari 26 na afisa wa kijeshi wa Israel dhidi ya miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani na kubainisha kuwa, mbali na njama za sasa za Wazayuni dhidi ya taifa hili, jeshi la Israel linajiandaa pia kufanya operesheni dhidi ya Iran likisisitiza kuwa chaguo hilo la kuishambulia kijeshi Iran 'lingalipo mezani.'
Mwanadiplomasia huyo wa Iran amekariri kuwa, ni haki ya Iran kujihami na kujibu vitisho na chokochoko zozote inazofanyiwa kama vile vitisho vinavyotolewa mara kwa mara na maafisa wa utawala wa Kizayuni.
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika UN ameongeza kuwa, vitisho hivyo vya utawala wa Kizayuni vinakiuka Kipengee cha 2 cha Hati ya Umoja wa Mataifa na kwamba jamii ya kimataifa inapaswa kutoa jibu mwafaka haswa kwa kutilia maanani kuwa, Tel Aviv ina faili jeusi la kuzishambulia nchi za eneo la Asia Magharibi.