Bunge la Ufaransa lapitisha sheria iliyo dhidi ya Uislamu
(last modified Wed, 17 Feb 2021 08:04:48 GMT )
Feb 17, 2021 08:04 UTC
  • Bunge la Ufaransa lapitisha sheria iliyo dhidi ya Uislamu

Bunge la Ufaransa jana Jumanne lilipitisha sheria iliyo dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa wabunge 347 waliunga mkono sheria hiyo na wengine 151 waliipinga na hivyo ilipitishwa kwa wingi wa kura. Sheria hiyo sasa itapelekwa katika Bunge la Senate ili ipigiwe kura ya mwisho na ikipita itaanza kutekelezwa.

Sheria hiyo ambayo imepewa jina la “Sheria ya Kuimarisha Thamani za Kijamhuri” inalenga kukabiliana na mambo kadhaa yanayowahusu Waislamu kama vile mafunzo ya kidini, mitandao na kuoa wake wengi.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amependekeza sheria hiyo kwa ajili ya kukabiliana na kile alichokitaja ni 'Uislamu wa wanaotaka kujitenga.'

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa Gerald Darmanin amedai katika ukurasa wake wa Twitter kuwa sheria hiyo inalenga kulinda thamani za jamhuri sasa na siku za usoni.

Maandamano ya kumpinga Rais Macron wa Ufaransa

Jumuiya ya Waislamu Ufaransa (CFCM) imepinga vikali sheria hiyo na kuitaja kuwa yenye kuwawekea Waislamu vizingiti katika maisha yao yote.

Sheria hiyo inaipa serikali haki ya kuingilia mambo ya misikiti na kupeleleleza kamati zinazosimamia misikiti na pia kudhibiti matumizi ya pesa za misikiti na asasi za Waislamu.

Hivi karibuni watu wa Ufaransa waliandamana na kusisitiza kuwa sheria hiyo itaweka vizingiti dhidi ya Uislamu ambayo ni dini ya pili kwa ukubwa nchini humo.

Katika miezi ya hivi karibuni Ufaransa imeshadidisha mbinyo dhidi ya Waislamu nchini humo ambapo hata maduka ya Waislamu yanafungwa kwa visingizio mbali mbali.