Zakharova: Biden anafuata siasa zile zile za Donald Trump
(last modified Sun, 21 Feb 2021 17:00:04 GMT )
Feb 21, 2021 17:00 UTC
  • Maria Zakharova
    Maria Zakharova

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia amejibu matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Rais wa Marekani kuhusu nchi hiyo akisema: Matamshi hayo ya Joe Biden hayana jipya na hayana tofauti hata kidogo na sera za serikali ya zamani ya Marekani.

Maria Zakharova amesema: "Matamshi ya Biden hayakuwa na jipya. Tunapaswa kukumbuka yaliyotokea mwaka jna, miaka miwili iliyopita na mwaka 2016; je, kuna tofauti yoyote katika mienendo ya Marekani?" Zakharova mesisitiza kuwa Joe Biden anatekeleza sera zile zile za serikali ya kabla yake. 

Katika hotuba yake kwenye mkutano wa usalama wa Munich, Rais wa Marekani amedai kuwa, Russia inafanya jitihada za kudhoofisha mpango wa Ulaya na muungano uliopo katika jumuiya ya NATO, na kwa sababu hiyo daima inazitia hofu nchi nyingine badala ya kufanya mazungumzo na jamii ya kimataifa.

Vilevile Biden ameituhumu Moscow kuwa imehusika na mashambulizi ya mtandaoni (cyber attaks) nchini Marekani na katika nchi za Ulaya.

Joe Biden

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia pia ameashiria kwamba kusajiliwa chanjo ya tatu ya kupambana na virusi vya corona nchini Russia na mafanikio makubwa ya chanjo ya corona ya Sputnik V katika upeo wa dunia havizifurahishi nchi za Magharibi na inatazamiwa kuwa siku zijazo zitashuhudia wimbi jipya la propaganda chafu dhidi ya Russia.  

Kinyume na miaka iliyopita, mara hii nchi za Russia na China hazikualikwa katika mkutano wa kila mwaka wa usalama wa Munich.