Italia: Tunaunga mkono juhudi za kuleta amani na utulivu nchini Libya
(last modified Fri, 12 Mar 2021 12:02:24 GMT )
Mar 12, 2021 12:02 UTC
  • Italia: Tunaunga mkono juhudi za kuleta amani na utulivu nchini Libya

Serikali ya Italia imesema kuwa inaunga mkono kikamilifu juhudi za kurejesha amani na utulivu katika nchi ya kaskazini mwa Afrika ya Libya.

Waziri Mkuu wa Italia, Mario Draghi, amesema hayo wakati alipofanya mazungumzo ya simu na waziri mkuu mwenzake wa Libya, Abdul Hamid Dbeibah na kusisitiza kuwa, Rome inaunga mkono kikamilifu juhudi za kurejesha na kudumisha amani na utulivu nchini Libya. Amesema, Italia inaunga mkono kulindwa umoja wa ardhi yote ya Libya na anaiomba serikali mpya ya nchi hiyo kuzingatia zaidi masuala ya kimsingi na yenye kipaumbele kikubwa kama ustawi na usalama wa wananchi wa Libya.

Waziri Mkuu wa Italia vile vile ametilia mkazo haja ya kuendelea kustawishwa na kuimarishwa uhusiano wa nchi mbili katika masuala yote yanayozihusu pande hizo mbili.

Waziri Mkuu wa Libya, Abdul Hamid Dbeibah 

 

Kabla ya hapo yaani siku ya Jumatano, Wizara ya Mambo ya Nje wa Italia ilielezea kufurahishwa na hatua ya bunge la Libya ya kuipasisha serikali mpya ya nchi hiyo chini ya Waziri Mkuu Abdul Hamid Dbeibah.

Jumanne wiki hii, Machi 10, 2021, Bunge la Libya lilipiga kura na kutangaza kuwa na imani na Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Waziri Mkuu Dbeibah. Wabunge wa pande hasimu nchini Libya  walikutana kuanzia Jumatatu katika mji wa Sirte kwa ajili ya kujadiliana serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyopendekezwa na Waziri Mkuu Abdul Hamid Dbeibah.

Serikali mpya ya Umoja wa Kitaifa ya Libya ina mawaziri 33 wakiwemo manaibu wawili wa waziri mkuu na wote wanawakilisha maeneo mbalimbali ya nchi hiyo kijiografia na pia kijamii.