UN: Mizozo imesababisha watu milioni 88 duniani wakabiliwe na njaa
Umoja wa Mataifa umesema makumi ya mamilioni ya watu katika pembe mbalimbali za dunia wanaandamwa na njaa na ukosefu wa usalama wa chakula kutokana na mizozo, migogoro na ukosefu wa uthabiti.
Kwa mujibu wa UN, kufikia mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2020, zaidi ya watu milioni 88 walikuwa wanasumbuliwa na ukosefu wa usalama wa chakula katika maeneo mbalimbali ya dunia, hilo likiwa ni ongezeko la asilimia 20 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres ametahadharisha kuwa, watu milioni 30 katika nchi zaidi ya 30 duniani wapo katika ncha ya kutumbukia katika baa la njaa iwapo hatua za dharura za kuwanusuru hazitachukuliwa.
Ametaja nchi ambazo zipo katika hatari kubwa ya ukosefu wa usalama wa chakula kuwa ni Ivory Coast, Sudan Kusini, Afghanistan na Yemen. Umoja wa Mataifa umeeleza wasiwasi ulionao wa uwezekano wa kuongezeka vifo duniani kutokana na vita, mizozo na kuenea virusi vya Corona.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP), Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) na Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa ujumla asilimia 10 ya watu duniani ambayo ni sawa na watu milioni 821.6 duniani kote wanakabiliwa na baa la njaa.
Aidha takwimu hizo zinaonesha kuwa, watu milioni 462 akthari yao wakiwa ni watoto wadogo wanaishi katika hali ya lishe duni na utapiamlo katika maeneo mbalimbali duniani.