Guterres alaani chuki dhidi ya Waislamu, anukulu aya ya Qur’ani
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu (Islamophobia) na kusema ubaguzi wa rangi kwa bahati mbaya sana upo na unaendelea katika nchi zote na katika jamii zote duniani na mizizi yake imekita kutokana na karne na karne za ukoloni na utumwa.
Gutteres ameyasema hayo kwa mnasaba wa maadhimisho ya kimataifa ya kupinga ubaguzi wa rangi yaliyofanyika kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Katika kikao hicho ambacho aghalabu ya washiriki walishiriki kwa njia ya intaneti, Gutteres alisema: “Tunauona ubaguzi ulioenea na kutengwa na kuteswa kwa watu wa asili ya Kiafrika. Tunauona katika dhuluma na ukandamizaji unaovumiliwa na watu wa kiasili na makabila mengine madogo.”
Hali kadhalika amebaini kuwa, “Tunauona katika maoni yenye kuchukiza ya wanaoona kuwa wazungu ni watu bora kuliko watu wengine na kwenye vikundi vingine vyenye msimamo mkali. Tunaona pia ubaguzi wa rangi na ubaguzi katika chuki dhidi ya Uyahudi, chuki dhidi ya Waislamu, unyanyasaji wa jamii ndogo za Kikristo na aina zingine za kutovumiliana na chuki dhidi ya wageni. Na tumeuona ubaguzi wa rangi katika vurugu za hivi karibuni za kuchukiza dhidi ya watu wa asili ya Asia, wanaolaumiwa bila haki kwa kusambaza COVID-19.”
Katika kusisitiza umuhumu wa wanadamu wote kuishi kwa pamoja Gutteres amenukulu sehemu ya aya ya 13 ya Sura Hujurat katika Qur’ani Tukufu inayosema: “Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane...”