Moscow: Iran ina nafasi muhimu katika kutatua masuala ya Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i68270-moscow_iran_ina_nafasi_muhimu_katika_kutatua_masuala_ya_afghanistan
Mjumbe Maalumu wa Russia katika Masuala ya Afghanistan amesisitiza umuhimu wa nafasi chanya ya Iran katika kuyapatia ufumbuzi masuala mbalimbali ya Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 24, 2021 22:06 UTC
  • Moscow: Iran ina nafasi muhimu katika kutatua masuala ya Afghanistan

Mjumbe Maalumu wa Russia katika Masuala ya Afghanistan amesisitiza umuhimu wa nafasi chanya ya Iran katika kuyapatia ufumbuzi masuala mbalimbali ya Afghanistan.

Zamir Kabulov jana alisema kuwa Iran inaweza kuwa na mchango muhimu iwapo itajiunga na mazungumzo ya Afghanistan. Kabulov amesema, kutokuwepo Iran kwenye meza ya mazungumzo ya Afghanistan kunahisika na kwamba inatarajikuwa, katika siku za karibuni, washirika wetu wa Irani watajiunga na jitihada hizi na kufanya kazi kwa nguvu zote katika uwanja huo ili kuyapatia ufumbuzi matatizo ya Afghanistan.  

Kuhusu vitisho vya kundi la Daesh huko kaskazini mwa Afghanistan, Kabulov amesema: vitisho hivyo vingali vinaendelea na kwamba Daesh bado ni hatari huko kaskazini mwa Afghanistan.  

Mjumbe Maalumu wa Russia katika Masuala ya Afghanistan ameashiria pia kwamba haoni tofauti kubwa kati ya serikali ya Donald Trump na ya sasa ya Joe Biden kuhusiana na masuala ya Afghanistan na kueleza kuwa: Russia haishuhudia mabadiliko mahsusi katika siasa za Marekani kuhusiana na Afghanistan baada ya kuingia madarakani Rais Joe Biden. 

Magaidi wa Daesh bado ni tishio kaskazini mwa Afghanistan 

Kikao cha siku moja kati ya wajumbe wa Marekani, Russia, China na Pakistan kuhusu Afghanistan kilifanyika Alhamisi iliyopita Machi 18 huko Moscow mji mkuu wa Russia, ambapo katika kikao hicho jumbe za serikali ya Afghanistan na kundi la Taliban pia zilihudhuria kikao hicho. 

Taarifa ya pamoja iliyotolewa mwishoni mwa kikao hicho ilieleza kuwa, kwa mujibu wa azimio nambari 2513 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la mwaka jana wa 2020 kuhusu kuhitimisha vita huko Afghanistan, nchi hizo haziungi mkono suala la kurejeshwa Imara ya Kiislamu nchini humo.  

Taarifa hiyo pia imelitaka kundi la Taliban lisitekeleze oparesheni za mashambulizi msimu wa machipuo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ili kuzuia mauaji ya raia.