Jengo la Congress la Marekani lafungwa kutokana na vitisho vya kiusalama
Vyombo vya habari vimetangaza kuwa, jengo la Congress ya Marekani limefungwa kutokana na vitisho vya kiusalama.
Jana Ijumaa, vyombo vya habari vya ndani na nje ya Marekani viliakisi kwa wingi habari ya gari moja kuvamia eneo la jengo hilo na kuua afisa mmoja wa polisi na kumjeruhi mwengine mmoja.
Televisheni ya CNN ya Marekani imetangaza kuwa, maafisa usalama wamelimiminia risasi gari hilo na kumuua dereva wake.
Picha zilizosambazwa kuhusu maeneo ya karibu na jengo la Congress zinaonesha idadi kubwa ya polisi na maafisa usalama waliomiminwa katika eneo hilo. Watu wote waliomo kwenye jengo hilo wametakiwa wakae kwenye sehemu zao na hata wasichungulie madirishani.
Tarehe 6 Januari mwaka huu pia wafuasi wa rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump walilivamia jengo la Congress na kufanya mauaji na uharibifu mkubwa.
Wafuasi wa Trump walilivamia jengo hilo baada ya rais huyo wa zamani wa Marekani kutuma ujumbe mbalimbali wa maandishi na video katika mitandao ya kijamii hasa Twitter na kuwachochea wafuasi wake wafanye fujo.
Watu wasiopungua 6 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa wakati wafuasi wa Trump walipolivamia jengo la Congress Jumatano ya tarehe 6 Januari 2021.
Trump alichukua hatua hiyo baada ya kuona njia zote za kubadilisha matokeo ya uchaguzi wa rais zimeshindikana. Uvamizi wa wafuasi wake hapo tarehe 6 Januari 2021 ulifanyika baada ya mabaraza mawili ya Congress, lile la Wawakilishi na lile la Senate kukutana ili kupasisha ushindi wa Joe Biden katika uchaguzi wa Rais wa Novemba 23, 2020 huko Marekani.