Kwa kuamua kuondoa wanajeshi wake, Marekani imekiri kushindwa kikamilifu Afghanistan
Mtaalamu mmoja wa masuala ya kisiasa nchini Pakistan amesema, uamuzi wa Marekani wa kuwaondoa wanajeshi wake nchini Afghanistan ni sawa na Washington kukubali kuwa imeshindwa mtawalia kwa muda wa miaka 20 ya kuwepo kwake kijeshi nchini humo.
An'amul-Haq, ameyasema hayo katika makala iliyochapishwa na gazeti la Express Tribune la nchini Pakistan kwa anuani ya "Afghanistan, simulizi ya kushindwa na kulazimika kuondoka Marekani" na kuongeza kuwa, katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, viongozi wa Marekani wamefanya kila waliloweza ili kuchelewesha mpango wa kuwaondoa wanajeshi wa nchi hiyo huko Afghanistan.
Mtaalamu huyo wa masuala ya kisiasa wa Pakistan ameongeza kuwa, Rais Joe Biden wa Marekani amekiri kushindwa kihistoria kwa nchi hiyo na kutoweza kurejesha amani na uthabiti nchini Afghanistan; na kwa muktadha huo ametangaza tarehe ya mwisho kwa askari wa Marekani kuondoka kikamilifu katika ardhi ya Afghanistan.
Mchakato wa askari wa jeshi la Marekani kuondoka nchini Afghanistan umepangwa kuanza mnamo siku nne zijazo.
Rais Joe Biden wa Marekani alitangaza hivi karibuni kuwa, ifikapo tarehe 11 ya mwezi ujao wa Mei wanajeshi wa nchi hiyo watakuwa wameshaondoka huko Afghanistan.
Mnamo mwaka 2001, Marekani na waitifaki wake waliishambulia na kuivamia kijeshi Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kurejesha amani nchini humo; hata hivyo uvamizi huo uliitumbukiza Afghanistan kwenye lindi la vita na mapigano, kuangamiza miundomsingi yake ya kiuchumi na kushamirisha machafuko, ugaidi na uzalishaji wa madawa ya kulevya katika nchi hiyo.../