Apr 29, 2021 02:21 UTC

Uchunguzi uliofanywa na wataalamu mashuhuri wa haki za binadamu kote dunia kuhusiana na ukatili wa polisi wa Marekani umebaini kuwa, mauaji yanayofanywa kwa mpangilio maalumu na ya kimfumo, na vitendo vya polisi vya kuwapiga na kuwanyanyasa Wamarekani weusi ni sawa na jinai dhidi ya binadamu ambavyo vinapaswa kuchunguzwa kwa kina na kufuatiliwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Kamisheni ya wataalamu 12 wa haki za binadamu kutoka nchi 11 wamesema katika ripoti yao yenye kurasa 188 kwamba, Marekani inahusika na ukiukaji wa muda mrefu wa sheria za kimataifa ambao wakati mwingine unafikia kiwango cha kutambuliwa kuwa ni jinai dhidi ya binadamu.

Wataalamu hao pia wameashiria mauaji yanayofanywa na polisi wa Marekkani na kuwanyima raia weusi uhuru wa kimwili, kuwatesa, kuwanyanyasa na matendo mengine ya kikatili yanayofanyika kwa mpangilio maalumu dhidi ya jamii ya Wamarekani weusi. 

Ripoti ya kamisheni hiyo imeweka wazi athari mbaya za ubaguzi wa kimfumo unaofanyika nchini Marekani dhidi ya raia wenye asili ya Afrika na kusema: Marekani ina mifumo ya aina mbili ya sheria, mmoja kwa ajili ya wazungu, na mwingine kwa ajili ya raia wenye asili ya Afrika.

Kamisheni hiyo pia imeituhumu Marekani kuwa inakiuka sheria za kimataifa za haki za binadamu katika sheria zake zinazotawala masuala ya polisi, na pia katika utendaji wa maafisa wa utekelezaji wa sheria ikiwa ni pamoja na kusimamisha magari kwa ajili ya kuwalenga Wamarekani weusi, kufanya taftishi na upekuzi kwa msingi wa mbari, utumiaji mbaya wa silaha za moto na nyezo za mateso dhidi ya watu weusi na kuwakingia kifua na kuwapa kinga maafisa wa polisi wanaohusika na uhalifu huo.

Kuchapishwa kwa ripoti hiyo muhimu ambayo ni matunda ya juhudi za wataalamu nguli wa masuala ya haki za binadamu kutoka nchi mbalimbali ni sisitizo na ithibati inayoonyesha jinai zinazofanywa na maafisa wa polisi wa Marekani dhidi ya raia wenye asili ya Afrika wa nchi hiyo; kiasi kwamba wataalamu hao wameutambua uhalifu huo kuwa ni sawa na jinai dhidi ya binadamu na wametoa wito wa jinai hizo kufuatiliwa na vyombo vya kimataifa hususan Makama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Ukatili na nyama usio na mpaka wa polisi wa Marekani ulimulikwa zaidi kimataifa baada ya mauaji yaliyofanywa na polisi mzungu, Derek Chauvin dhidi ya raia mweusi wa nchi hiyo, George Floyd hapo tarehe 25 Mei mwaka jana katika mji wa Minneapolis kwenye jimbo la Minnesota. Mauaji hayo yalifuatiwa na maandamano makubwa ya miezi kadhaa katika miji yote ya Marekani na katika nchi mbalimbali duniani. Maandamano hayo yalifanyika katika kalibu ya malalamiko ya walimwengu yaliyotolewa chini ya anwani ya Black Lives Matter (BLM) (maisha ya watu weusi yana tahamani). Vikao vya mahakama inayoshughulikia kesi hiyo viliendelea kwa muda wa karibu wiki tatu, na tarehe 20 mwezi huu wa Aprili jopo la majaji wa mahakama hiyo lilimpata afisa wa polisi Derek Chauvin na hatia ya mauaji.

Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kukabiliana na Mateso, (World Organisation Against Torture) Hina Jilani anasema: "Hukumu iliyotolewa dhidi ya muuaji wa George Floyd imethibitisha mitazamo ya shirika hili." Jilani ameongeza kuwa: "Hukumu hii imethibitisha kwamba, kutumia nguvu kubwa wakati wa kumtia nguvuni mtuhumiwa si kitendo cha kibinadamu, bali ni kielelezo cha waziwazi cha mateso na kunasababisha kifo."

Nukta ya kushangaza hapa ni kwamba, hukumu ya mahakama ya Marekani iliyompata na hatia ya mauaji polisi huyo mzungu, imekosolewa na viongozi wa chama cha Republican. Suala hili linaonyesha jinsi viongozi wa ngazi za juu wa Marekani, nchi inayodai kutetea haki za binadamu na demokrasia, wanavyotetea na kumkingia kifua polisi mtenda jinai ambaye alimuua kwa damu baridi, kikatili na bila ya sababu ya maana raia mweusi wa nchi hiyo.

Ukatili na manyanyaso ya vyombo vya dola dhidi ya raia weusi wa Marekani umeshadidi zaidi hususan katika kipindi cha rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump. Takwimu zinaonyesha kuwa, uwezekano wa polisi kumuua Mmarekani mweusi ni mara tatu zaidi ya raia mzungu. Uchunguzi unaonyesha kuwa, ukatili unaochochewa na ubaguzi wa rangi wa wazungu wenye itikadi za kifashisti huko Marekani hilenga zaidi jamii za waliowachache kidini na kimbari kama Wamarekani weusi, na polisi wazungu wenye mitazamo ya kibaguzi wamekuwa na mkono mrefu zaidi katika mauaji na ukatili huo.

Alaa kulli hal, ripoti iliyotolewa na wataalamu mashuhuri wa haki za binadamu wa nchi 11 duniani inaonyesha kuwa, ukatili usio na mpaka na mauaji yanayofanywa na polisi wa Marekani dhidi ya raia wenye asili ya Afrika wa nchi hiyo vinapaswa kufuatiliwa katika ngazi ya kimataifa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kama jinai dhidi ya binadamu.            

Tags