Feb 24, 2024 09:19 UTC
  • Mtazamo wa kiusalama wa maadui kuhusu uchaguzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Ufuatiliaji na uchunguza wa mienendo na harakati za maadui kuhusu uchaguzi wa Machi Mosi nchini Iran unaonyesha kuwa wanautazama uchaguzi huo wa Bunge kwa mtazamo wa kiusalama.

Duru ya kumi na mbili ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Jamhuri ya Kiislamu na ya sita ya uchaguzi wa Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Iran itafanyika Ijumaa ijayo, Machi Mosi.

Katika miaka ya hivi karibuni, sera kuu na muhimu zaidi ya maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa kuzusha migogoro ya ndani na kuibua pengo kati ya wananchi na serikali. Lengo muhimu zaidi la Marekani kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuiwekea Iran vikwazo vipya kuanzia mwaka 2018 na kuendelea, lilikuwa kuwawekea mashinikizo wananchi katika masuala ya kimaisha na kugeuza hali ya kutoridhika wananchi kuwa mgogoro wa kiusalama na hatimaye kuanzisha machafuko dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Ghasia na machafuko ya mwaka jana nchini Iran ni miongoni mwa matukio ambayo yaliungwa mkono na kufadhiliwa na maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ambao walifanya juu chini kuyaendeleza kwa miezi kadhaa.

Makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yaliyopasishwa na Baraza la Usalama la UN 

Moja ya sababu kuu za sera hizo ni kushindwa kuilazimisha Jamhuri ya Kiislamu ifuate siasa za kigeni za nchi za Magharibi na kutokuwa huru katika kufanya maamuzi ya sera za kigeni. Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikataa kutupilia mbali uhuru wake katika kuchukua maamuzi ya sera za kigeni na kwenda sambamba na maslahi ya nchi za Magharibi hususan Marekani, hata katika kipindi cha mashinikizo makubwa zaidi ya vikwazo.

Hivi sasa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa mbioni kufanya uchaguzi wa 12 wa Bunge na wa 6 wa Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ambazo ni chaguzi za 40 na 41 katika kipindi cha miaka 45 iliyopita, tunashuhudia muendelezo wa sera za maadui za kuyatazama matukio ya kisiasa nchini Iran kwa jicho la kiusalama. Kwa hakika, maadui wanafanya mikakati ya kuanzisha uhusiano kati ya vikwazo, ghasia na uchaguzi na kutaka kuona matokeo ya sera na mienendo yao ya kihasama ya miaka iliyopita kwenye masanduku ya kupigia kura. Kwa hivyo, wanachotarajia kukiona katika uchaguzi wa Ijumaa ijayo ni kususia na ushiriki mdogo wa wananchi. Kwa msingi huo, wameanzisha propaganda kubwa za kuhoji umuhimu wa uchaguzi wa Bunge wakiwahimiza watu kususia na kutoshiriki uchaguzi huo.

Miaka 45 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu 

Miongoni mwa malengo ya sera hizo ni kupunguza au kufuta uhalali wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika mkondo huo, Imamu wa Swala ya Ijumaa ya jana mjini Tehran, Hujjatul-Islam Walmuslimin Mohammad Javad Haj Ali Akbari alisema katika hotuba za Swala hiyo kwamba: "Maadui na mrengo mzima unaopinga Mapinduzi ya Kiislamu na Iran chini ya bendera ya kufuru ya kimataifa, wamepeperusha bendera ya kupinga uchaguzi wa Iran, na zaidi ya mitandao na vituo 500 vya televisheni vinaeneza propaganda chafu dhidi ya uchaguzi huo."

Maadui wa utawala wa Kiislamu nchini Iran wamefikia hitimisho kwamba, uungaji mkono wa wananchi na mtaji wa kijamii ndio chanzo muhimu zaidi cha nguvu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambao walitamani mfumo wa Kiislamu wa Iran usiuone mwaka wa 40 wa uhai wake na sasa imekamilisha umri wa miaka 45, wamejikita zaidi katika kutenganisha wananchi na utawala na hivyo kutumia vyombo vya habari, kutangaza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepoteza mtaji wake wa kijamii na uungaji mkono wa waliowengi. Hata hivyo njama hii, kama zilivyokuwa za miaka iliyopita, itafeli na kugonga mwamba kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na nguvu na irada ya wananchi shupavu wa Iran ya Kiislamu.

Tags