Feb 17, 2024 09:24 UTC
  • Sababu za maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupiga upatu wa kuwachochea wananchi wasusie uchaguzi

Wiki mbili zimebakia hadi kufanyika uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu na wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusimamia kazi zake. Jambo hilo limepelekea maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuzidisha propaganda zao za kuwachochea wananchi wasusie uchaguzi huo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amezungumzia mikakati minne, ambayo ni kuwepo ushindani wa kweli, kufanyika uchaguzi safi, kuwepo usalama kamili na kushiriki kwa wingi na kwa shauku wananchi katika upigaji kura wa uchaguzi huo utakaofanyika tarehe Mosi Machi. Mkabala na mikakati hiyo minne, maadui wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanaeneza sumu ya kutilia shaka kuwepo ushindani wa kweli na kufanyika uchaguzi safi ulio huru na wa haki; na hivyo kuwataka wananchi wasusie uchaguzi huo. Hata hivyo, hatua hiyo ya maadui ina mgongano ndani yake, kwa sababu kwa upande mmoja, wanauelezea uchaguzi kuwa ni wa mapambo na wa kimaonyesho tu na kwa hivyo hauna umuhimu wowote, lakini kwa upande mwingine, wanatumia nyenzo zote walizonazo kuwashawishi wananchi wasijitokeze kwenda kupiga kura. Lakini ni kwa nini maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanahangaika na kufanya hila na njama zote hizo?

Sababu ya kwanza ni kuwa kimsingi maadui wanafahamu vyema kwamba, uchaguzi nchini Iran hauchukuliwi kuwa ni kitu cha pambo na cha kimaonyesho, bali ni uwanja unaotoa fursa ya kupokezana madaraka kwa njia za amani. Kile ambacho kimekuwa kikifuatiliwa na maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miaka ya hivi karibuni ni kuandaa mazingira ya kuzusha machafuko na ghasia nchini, wakati kufanyika uchaguzi ni hatua ya kukabiliana na lengo hilo.

Uchaguzi wa Iran

Sababu ya pili ni kuwa, kama alivyoeleza Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi, uchaguzi huwa sababu ya kupatikana umoja wa kitaifa; na umoja huo hupelekea kuwepo usalama wa kitaifa, na usalama wa kitaifa ndio unaolifanya taifa lenyewe liwe imara na lenye nguvu. Kwa upande mmoja, maadui wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hawataki kuwepo umoja wa kitaifa; na kwa upande mwingine hawapendi kuona Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unakuwa imara na wenye nguvu. Maslahi ya maadui hao yanapatikana kwa kuzusha hitilafu na mifarakano baina ya wananchi, na kwa kudhoofisha nguvu na nafasi ya ndani na nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa hivyo, kila unapofanyika uchaguzi nchini Iran hususan katika kipindi cha muongo mmoja sasa, maadui hupiga ngoma ya kususiwa uchaguzi; na mara hii suala hilo linafuatiliwa kwa nguvu na uzito mkubwa zaidi kulinganisha na mara nyinginezo, kwa sababu maadui hawakuweza kufikia malengo yao dhidi ya Mfumo wa Kiislamu kupitia fujo na machafuko waliyochochea nchini mwaka uliopita, na kwa hivyo, hivi sasa wanajaribu kuutia dosari uhalali wa kisiasa na kukubalika kwa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuwashawishi wananchi wasishiriki katika uchaguzi.

uchaguzi nchini Iran

Sababu ya tatu ni kwamba katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni maadui wamekuwa wakiilenga rasilimali ya kijamii ya Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hata kushadidishwa vikwazo pia kunafanyika kwa lengo la kuwawekea mashinikizo ya kiuchumi wananchi ili wanung'unike na kuonyesha kuwa hawaridhishwi na Mfumo wa uongozi. Kutokana na kubainisha hali halisi ilivyo kiidadi na kitarakimu badala ya makisio na makadirio tu, uchaguzi ni miongoni mwa njia zinazowezesha kuzima mbinu za kipropaganda za maadui. Wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambao hawakuwa na matumaini ya kuuona Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unafikisha umri wa miaka 40, hivi sasa wameelekeza nguvu zao zote kupitia mtandao wao wenye nguvu wa vyombo vya habari katika kuwalenga wananchi ili kuwatenganisha na Mfumo na kuonyesha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepoteza rasilimali yake ya kijamii ya msukumo na uungaji mkono wa wananchi. Kuwashawishi wananchi wasishiriki katika uchaguzi nako pia inapasa kutathminiwe katika mtazamo huo.

Na sababu ya nne ya kuwashawishi wananchi wasishiriki katika uchaguzi ni kutaka kudhoofisha nafasi ya Serikali na Bunge kieneo na kimataifa. Wapinzani wanaamini kuwa kadiri ushiriki wa wananchi katika uchaguzi utakavyokuwa wa kiwango cha chini ndivyo Serikali na Bunge zitakavyokuwa na nafasi dhaifu na ushawishi mdogo zaidi kieneo na kimataifa na hivyo kuwa na sauti ya chini katika kufuatilia na kutetea maslahi ya taifa.

Tags