May 12, 2021 00:47 UTC
  • UN: Kundi la Daesh lilifanya jitihada za kuangamiza Waislamu wa madhehebu ya Shia

Mkuu wa timu ya Umoja wa Mataifa iliyopewa jukumu la kuchunguza jinai na uhalifu uliofanywa na kundi la kiwahabi la Daesh amesema kuwa, kundi hilo la kigaidi lilifanya jitihada za kuangamiza Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Karim Ahmad Khan amesema katika ripoti yake kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba, timu ya uchunguzi imegundua kwamba, mashambulizi ya Daesh dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia waliokuwa katika Academia ya Jeshi la Anga la Iraq huko Tikrit yaliambatana na mauaji, ukatili, mateso na manyanyaso ya kutisha dhidi ya ubinadamu.

Ripoti hiyo ya timu ya Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, uchunguzi umebaini kwamba, kundi la Daesh lilifanya juhudi za kuangamiza Waislamu wa madhehebu ya Shia.

Timu hiyo ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa iliundwa Septemba mwaka 2017 kwa mujibu wa azimio nambari 2379 la Baraza la Usalama ili kufuatilia jinai na uhalifu uliofanywa na kundi la kigaidi la Daesh.

Timu hiyo inasaidia jitihada za kuwashughulikia wanachama wa kundi hilo la kiwahabi waliotenda jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu.

Katika kampeni za uchaguzi wa rais mwaka 2016, aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump aliitaja serikali ya Barack Obama kuwa ndiyo iliyoanzisha kundi la kigaidi la Daesh. Katika hotuba yake ya Januari 2016, Donald Trump alisema: "Obama na Hillary Clinton ndio waliounda kundi la Daesh.

Mwaka 2017 Iraq ilitangaza kulishinda kundi la Daesh baada ya kupigana nalo vita kwa muda wa miaka mitatu. Hata hivyo mamluki na masalia ya kundi hilo la kitakfiri bado wametapakaa huku na kule wakitenda jinai na kufanya hujuma za kushtukiza dhidi ya raia wa Iraq katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Diyala, Kirkuk, Nainawa, Salahuddin, al Anbar na mji mkuu, Baghdad.

Tags