Indhari ya Shirika la Afya Duniani kuhusu 'apartheid (ubaguzi) ya chanjo'
Katika hali ambayo, maradhi ya Covid-19 yameendelea kuua watu katika pembe mbalimbali za duniani, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ameashiria hali ya kusikitisha ya usambazaji chanjo ya kukabiliana na virusi vya corona na kusema kwamba, kwa bahati mbaya ulimwengu umeingia katika hatua ya 'apartheid (ubaguzi) ya chanjo.'
Filihali, kuenea virusi vya Corona ndio changamoto kubwa zaidi inayoyakabili mataifa ya dunia. Wimbi jipya la maradhi haya limeifanya hali ya mambo kuwa ngumu kwa wote. Mbali na mgogoro katika sekta ya tiba, dawa, vifaa vya matibabuu, hasa za kiuchumi na kijamii zilizosababishwa na Covid-19 ambazo ni kubwa kuliko ilivyotabiriwa, tatizo lilijitokeza kwa sasa, ni ugavi usio wa kiadilifu wa chanjo ya corona hususan hatua ya baadhi ya madola makubwa na tajiri ya kununua na kujilimbikizia chanjo hiyo.
Hatua ya madola hayo imeyanyima fursa mataifa mengine hususan masikini kupata chanjo hiyo ya corona. Kwa mujibu wa takwimu zilizosambazwa ni kuwa, hadi sasa zaidi ya watu 3,400,000 wameaga dunia kwa virusi vya Corona katika maeneo mbalimbali duniani.
Hii ni katika hali ambayo, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilianzisha mpango wa COVAX wa kugawa kiadifu chanjo ya corona katika maeneo yote ya dunia na kuyataka mataifa tajiri yatenge hisa kwa ajili ya mpango huu ili kuzisaidia nchi masikini. Lakini madola hayo siyo tu kwamba, yamekataa kutekeleza takwa hilo, bali yamechukua hatua isiyo ya kibinadamu ya kujilimbikiza chanjo ya Corona.
Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, takribani dozi milioni 900 zimeshatumika kuwadunga watu katika maeneo tofauti ya dunia ambapo asilimia 81 ya udungaji wa chanjo hiyo inahusiana na mataifa yenye kipato kikubwa au kipato cha kati kuelekea juu. Takwimu hizi zinasikitisha zaidi pale inapodhihirika kwamba, vitendo vya madola hayo ni 'apartheid (ubaguzi) ya chanjo' na ugaidi wa dawa.
Katika uwanja huo, Marekani na baadhi ya madola ya Ulaya licha ya kuwa na chanjo za ziada, lakini haziko tayari kushiriki katika mpango wa kutuma chanjo kwa mataifa mengine. Madola hayo yamejiwekea akiba ya dozi za chanjo ambayo ni zaidi ya idadi na wakazi wa mataifa hayo. Marekani, Umoja wa Ulaya, Uingereza, Australia, Canada na Japan hadi sasa zimejilimbikizia dozi zaidi ya bilioni 3 za Covid-19. Idadi hii ya dozi za Corona ni zaidi ya mahitaji ya raia wote wa mataifa hayo.
Hua Chunying, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China anasema: Katika hali ambayo, Marekani inaunda asilimia 4 ya wakazi wote wa dunia, serikali ya nchi hiyo imejilimbikizia karibu robo ya dozi zote za Corona.
Agnes Calamard, Katibu Mkuu wa Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International sambamba na kutoa mwito wa kuharakishwa ugavi wa chanjo ya corona amesema kuwa, kusambaa virusi vya corona kumefichua kutokuwa na uwezo ulimwengu wa kuwa na ushirikiano athirifu na wa kiadilifu, kiasi kwamba, nchi tajiri duniani zimehodhi chanjo ya corona, na kuzitelekeza nchi masikini ambazo zinakabiliwa na mgogoro mbaya zaidi wa kiafya na haki za binadamu.
Hali hii inashuhudiwa hata baina ya mataifa ya Ulaya ambayo ni wanachama wa Umoja wa Ulaya, kiasi kwamba, nchi hizo zimejitokeza na kulalamikia kutokuweko usawa katika ugavi wa chanjo ya corona. Sebastian Kurz, Kansela wa Austria sambamba na kuutaja ugavi wa chanjo ya corona kwamba, sio wa kiadilifu katika Umoja wa Ulaya amesema kuwa, baadhi ya nchi wanachama wa umoja huo zimepokea dozi nyingi zaidi ikilinganishwa na wanchama wengine.
Ngozi Okonjo-Iweala, Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani sambamba na kuyatahadharisha mataifa tajiri duniani amesema: Endapo nchi hizo zitasitasita katika kuzipatia nchi masikini chanjo ya corona, jambo hilo litakuwa na matokeo mabaya.
Pamoja na miito na matakwa yote hayo kuhusiana na jambo hilo, lakini mataifa tajiri na yenye nguvu duniani yameendelea kutanguliza mbele maslahi yao na kufanya mambo kinyume kabisa na nara zao za kuheshimu utu na ubinadamu ambapo hatua yao ya kujilimbikizia chanjo ya corona, kutotoa ushirikiano kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) na kuitumia chanjo hiyo kama wenzo wa kisiasa kivitendo yameeneza 'apartheid (ubaguzi) ya chanjo' na ugaidi na gaidi wa kimatibabu.