Chuki dhidi ya Uislamu: Msikiti mwingine wavunjiwa heshima nchini Uhispania
Msikiti mmoja umevunjiwa heshima nchini Uhispania ikiwa ni muendelezo wa chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya.
Shambulio dhidi ya msikiti huo limetokea katika mji wa Murcia ambapo watu wenye chuki na Uislamu waliandika katika kuta za msikiti huo maneno kama: Uislamu hapana, mamlaka ya kujitawala Uhispania si ya kufanyiwa mazungumzo.
Aidha watekelezaji wa kitendo hicho ambacho ni kinyume kabisa na uhuru wa kuabudu waliweka nje ya msikiti huo kichwa kilichokatwa cha nguruwe pamoja na kisu chenye damu.
Tukio hilo linatajwa kuwa wimbi jipya la hujuma na mashambulio ya chuki dhidi ya Uislamu katika eneo la Murcia lililoko kusini mwa Uhispania, eneo ambapo linatambulika kwa kuwa na wahajiri wengi.

Matukio ya hujuma na mashambulio ya chuki dhidi ya Uislamu yameongezeka mno barani Ulaya katika miaka ya hivi karibuni.
Katika kipindi cha uongozi wake nchini Marekani, Donald Trump alitoa matamshi na kuchukua hatua ambazo zinatathminiwa na wajuzi wa mambo kuwa zimekuwa na nafasi kubwa katika kueneza ubaguzi na misimamo ya kufurutu ada hususan chuki dhidi ya Uislamu.
Kivitendo ni kuwa, misimamo ya Donald Trump imeeneza miamala na vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya Waislamu.