Jamii ya Waislamu wa Canada yametangaza mshikamano na Wacanada asilia
Maimamu 75 wa misikiti ya Waislamu wa Canada wamekutana na raia asili wa nchi hiyo na kueleza mshikamano wao na jamii hiyo kutokana na kugunduliwa makaburi ya umati ya watoto wa Wacanada asili waliokuwa wakishikiliwa katika shule za Wamishonari wa Kikatoliti.
Ripoti zinasema kuwa, Imam wa Msikiti wa London katika jimbo la Ontario, Aarij Anwer amesema kuwa, Waislamu wote wanahisi mashaka ya jamii ya Wacanada asilia kwa sababu wanaelea vyema yaliyofanywa na ubeberu katika nchi zao.
Aarij Anwer ni mmoja kati ya maimamu 75 wa misikiti ya Canada ambo Ijumaa iliyopita walitangaza mshikamano wao na wenyeji wa nchi hiyo kutokana na maafa yaliyowapata maelfu ya watoto wao waliokuwa katika shule za bweni za Wamishonari wa Kikatoliki.
Msimamo huo wa maimamu wa misikiti ya Waislamu wa Canada umetangazwa baada ya kugunduliwa makaburi yenye maiti za zaidi ya watoto elfu moja waliokuwa wakishikiliwa katika shule za kidini za Kikatoliki.
Tangu mwezi Mei mwaka huu hadi sasa, kumegunduliwa maeneo manne yenye makaburi ya miili ya watoto hao wa shule za bweni za huko British Colombia, Saskatchewan na Manitoba. Mabaki ya miili ya watoto wasiopungua 1148 imepatikana katika kaburi la umati na makaburi mengine kadhaa yasiyo na majina ya watoto waliozikwa ndani yake.
Ripoti ya Kamati ya Ukweli na Maridhiano ya mwaka 2015 imeonyesha kuwa, watoto wasiopungua 4,100 waliuliwa wakiwa katika shule za bweni za Wamishonari wa Kikatoliki au kutoweka.

Ripoti hiyo ilifichua unyanyasaji wa kutisha wa kimwili, ubakaji, utapiamlo na unyama mwingine uliowapata watoto wengi anokadiriwa kufikia 150,000 waliohudhuria shule hizo, ambazo zilikuwa zikiendeshwa na makanisa ya Kikristo kwa niaba ya serikali ya Ottawa.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis amesema kuwa, ripoti iliyotolewa inatia uchungu lakini bado hajaomba rasmi rasmi kwa niaba ya Kanisa Katoliki.