Masharti ya Maduro kwa ajili ya kufanya mazungumzo na wapinzani
(last modified Wed, 14 Jul 2021 08:38:08 GMT )
Jul 14, 2021 08:38 UTC
  • Masharti ya Maduro kwa ajili ya kufanya mazungumzo na wapinzani

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ametangaza kuwa yupo tayari kufanya duru nyingine ya mazungumzo na wapinzani wa serikali iwapo baadhi ya masharti aliyotoa yatatimizwa.

Maduro ametoa masharti matatu ili mazungumzo hayo yafanyike na kusema: Jambo la kwanza ni kuwa Marekani na  Umoja wa Ulaya zinapasa kuiondolea Venezuela vikwazo; la pili, viongozi wa nchi hiyo wanapasa kutambuliwa na pande zote za kisheria na tatu, pande zote zinapasa kujizuia kutekeleza njama yoyote ya jinai kama mapinduzi dhidi ya watu wa Venezuela. 

Kutangazwa kuwa tayari Rais wa Venezuela kufanya mazungumzo na wapinzani ili kupunguza mivutano ya kisiasa katika nchi hiyo tajiri kwa mafuta ya Amerika ya Latini kunaonyesha nia njema aliyonayo na pia kuwaondolea kisingizio wapinzani khususan Juan Guaido kiongozi wa wapinzani cha kuituhumu serikali ya Venezuela kuwa haiafiki suala la kufikia mapatano. Maduro amechukua msimamo wake huo wa karibuni na  kutangaza kuwa tayari kufanya mazungumzo na wapinzani sambamba na kutilia maanani hatua za karibuni za nchi za Magharibi kuhusu Venezuela. Marekani na Umoja wa Ulaya tarehe 25 Juni mwaka huu zilitoa taarifa ya pamoja na kutangaza kuwa ziko tayari kutazama upya vikwazo dhidi ya Venezuela iwapo nchi hiyo itapiga hatua katika kuendesha kile zilichokitaja kuwa uchaguzi halali. Wakati huo huo Washington Jumatatu wiki hii iliipunguzia Venezuela vikwazo ilivyowekewa wakati wa utawala wa Trump na kuyaruhusu makampuni ya nje kuiuzia gesi nchi hiyo.  

Licha ya msimamo huo wa Maduro ambao umedhihirisha nia yake njema ili kuhitimisha mgogoro wa kisiasa huko Venezuela na pia kupunguza vikwazo vya Magharibi, lakini kwa kuzingatia rekodi ya misimamo ya Juan Guaido ambaye siku zote anapinga suala la kufanyika mazungumzo ili kufikiwa mapatano ya kitaifa; na wakati huo huo kutoa masharti yasiyotekelezeka katika uwanja huo, hakuna matarajio makubwa kwamba kiongozi huyo wa upinzani ataonyesha nia njema kwa serikali ya mrengo wa kushoto ya Venezuela na kukubali masharti ya Rais Maduro yaani kuitambua rasmi serikali ya Venezuela na kuachana na njama na juhudi za kuipindua serikali hiyo. 

Juan Guaido, kiongozi wa upinzani Venezuela 

Juan Guaido kiongozi wa upinzani wa Venezuela Januari 23 mwaka 2019 alijitangaza kuwa Rais wa Venezuela na Marekani ikamtambua rasmi mara moja baada ya tangazo hilo. Guaido anafanya kila awezalo kupitia Marekani ili kushika hatamu za uongozi nchini Venezuela. Marekani ni miongoni mwa nchi za awali kabisa zilizomuunga mkono Guaido na kuipinga serikali ya Venezuela. Ilizitaka nchi zote za dunia zimtambue rasmi kiongozi huyo wa upinzani kama rais halali wa Venezuela. Hakuna shaka kuwa katika miaka ya karibuni  Venezuela imekumbwa na hujuma na njama za Marekani na wapinzani wa ndani chini ya uongozi wa Juan Guaido zikiwemo njama za kutekeleza mapinduzi na kuibua machafuko na hali ya mchafukoge nchini humo. Lengo la Washington na vibaraka wake lilikuwa ni kumpindua Rais halali wa Venezuela  Nicolas Maduro na kuiingiza madarakani serikali kibaraka na yenye mielekeo ya Kimagharibi. Hadi Alami Fariman, mchambuzi wa mambo ya Amerika ya Latini anasema: Guaido atashindwa tu hata kama atafanikiwa kuunda serikali katika mazingira yasiyoweza kufikirika madhali alishindwa chini ya muungano wa kisiasa kuandaa mazingira mazuri na kutatua matatizo ya wananchi wa Venezuela.   

Wakati huo huo, Marais mbalimbali wa  Marekani tangu miaka 20 iliyopita hadi sasa wameiwekea Venezuela vikwazo vikali zaidi katika nyanja mbalimbali vikiwemo vikwazo vya kiuchumi kwa lengo la kuidhoofisha Venezuela na kuipindua serikali ya mrengo wa kushoto ya nchi hiyo. 

Washington ilianza kutekeleza mashinikizo na kuvuruga uchumi wa Venezuela tangu wakati wa utawala wa mwendazake Rais Hugo Chavez wa nchi hiyo; na mashinikizo hayo yangali yanaendelea hadi sasa wakati huu wa utawala wa Rais Nicolas Maduro. Hatua za Washington katika serikali ya sasa ya Marekani chini ya uongozi wa Rais Joe Biden wa chama cha Democrat pia zimejikita katika jitihada zenye lengo la kuipindua serikali huru na inayopinga ubeberu ya Venezuela na wakati huo huo ikiendelea kumuunga mkono kiongozi wa upinzani Juan Guaido. Serikali ya Biden awali ilidai kuwa imekusudia kufanya mazungumzo na kuanzisha uhusiano na serikali ya Venezuelana badala ya kuwaunga mkono waziwazi wapinzani na kuwa pamoja na Guaido, lakini sasa hatua yake ya kumtambua rasmi tena Guaido kama kiongozi wa wapinzani Venezuela na hata kumkabidhi mamilioni ya dola fedha za Venezuela ambazo zilikuwa zimezuiwa huko Marekani, kwa mara nyingine imezidisha chuki na uhasama wa serikali ya Washington kwa Maduro na serikali yake ya mrengo wa kushoto. 

Rais Joe Biden wa Marekani  

 

Tags