Mafuriko yaua makumi ya watu Afghanistan, 150 hawajulikani waliko
(last modified Fri, 30 Jul 2021 12:35:54 GMT )
Jul 30, 2021 12:35 UTC
  • Mafuriko yaua makumi ya watu Afghanistan, 150 hawajulikani waliko

Makumi ya watu wamepoteza maisha huku wengine wengi wakitoweka kutokana na mafuriko makubwa yaliyoikumba Afghanistan.

Saeedullah Nuristani, Mkuu wa Baraza la Mkoa wa Nuristan amesema mbali na watu 40 kuaga dunia kutokana na mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini humo, lakini wengine 150 hawajulikani walipo katika eneo hilo lililoko kaskazini mashariki mwa mji mkuu, Kabul.

Amesema nyumba zaidi ya 80 zimesombwa na maji ya mafuriko hayo katika eneo hilo liliko umbali wa kilomita 200 kaskazini mashariki mwa Kabul.

Naye Saeed Momand, Msemaji wa Gavana wa mkoa wa Nuristan amesema taarifa walizonazo ni kwamba, idadi ya watu walioaga dunia kufikia sasa kutokana na mafuriko hayo ni watu 60.

Maporokomo ya udongo yaliyosababishwa na mafuriko Afghanistan

Mwaka jana, makumi ya watu walifariki dunia pia kutokana na mafuriko yaliyoshuhudiwa katika mkoa wa Parwan, wakati wa msimu wa mvua za masika nchini Afghanistan.

Hii ni katika hali ambayo, idadi ya watu waliopoteza maisha kwa janga la mafuriko katika jimbo la Maharashtra nchini India imefikia 149 huku makumi ya watu wakiwa bado hawajulikani walipo.