Marekani yaachana na mpango wa kununua 'Ngao ya Chuma' ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i73972-marekani_yaachana_na_mpango_wa_kununua_'ngao_ya_chuma'_ya_israel
Jeshi la Marekani limeachana na mpango wake wa kununua mifumo mingine ya ngao ya makombora ya utawala haramu wa Israel, baada ya kuufanyia majaribio mfumo wa kutungua maroketi na makombora ya mafasa mafupi kutoka Tel Aviv mwanzoni mwa msimu huu wa joto kali; na kupata matokeo yasiyoridhisha.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 27, 2021 03:22 UTC
  • Marekani yaachana na mpango wa kununua 'Ngao ya Chuma' ya Israel

Jeshi la Marekani limeachana na mpango wake wa kununua mifumo mingine ya ngao ya makombora ya utawala haramu wa Israel, baada ya kuufanyia majaribio mfumo wa kutungua maroketi na makombora ya mafasa mafupi kutoka Tel Aviv mwanzoni mwa msimu huu wa joto kali; na kupata matokeo yasiyoridhisha.

Kwa mujibu wa ripoti iliyoandikwa na tovuti ya habari za ulinzi ya 'Defense News' Washington imeamua kununua ngao ya makombora kutoka kampuni ya Kimarekani ya Dynetics, baada ya kuufanyia majaribio mfumo huo pamoja na ule wa 'Iron Dome' wa Israel katika jimbo la New Mexico, kusini magharibi mwa Marekani mwezi uliopita, ili kujua upi bora.

Wizara ya Vita ya utawala haramu wa Israel, pamoja na kampuni ya Kizayuni inayozalisha mfumo huo ya 'Rafael Advanced Defense Systems' zimekataa kuzungumza chochote kuhusiana na ripoti hiyo, zilipotakiwa kufanya hivyo na gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post.

Wajuzi wa mambo wanasema uamuzi huo wa Marekani wa kuisusia ngao hiyo ya makombora ya Israel kutokana na udhaifu wake ni pigo kubwa kwa utawala pandikizi wa Israel, ambao daima umekuwa ukiupigia debe na kuunadi mfumo huo, licha ya kufeli mara kadhaa kutungua hata maroketi yanayovurumishwa kutoka Ukanda wa Gaza.

Ngao ya makombora ya Israel mkabala wa makombora ya Hamas

Hii ni katika hali ambayo, Aprili mwaka huu, kombora lililotokea Syria lilifanikiwa kuvuka ngao  dhidi ya makombora ya utawala wa Kizayuni wa Israel ambayo ni maarufu kama  'Kuba la Chuma' na kutua karibu na kituo cha siri na cha kistratijia cha nyuklia cha Dimona.

Kwa mujibu wa makubaliano ya mauzo ya 2019, jeshi la US lilinunua mifumo miwili ya ngao hiyo ya makombora, wa kwanza ukipelekwa nchini Marekani mwishoni mwa mwaka jana, huku wa pili ukiwasili Januari mwaka huu, kwa thamani ya dola milioni 373. Machi mwaka huu, Washington ilisema itatazama upya ununuzi zaidi wa mfumo huo wa Wazayuni, eti kwa kuwa hauoani na mfumo wa makombora wa Marekani.