Askari wa Marekani watuhumiwa kuua raia katika shambulio la Kabul
Baadhi ya raia wa Afghanistan miongoni mwa makumi ya watu waliopoteza maisha katika mkanyagano na fujo lililotokea nje ya Uwanja wa Ndege wa Kabul nchini Afghanistan baada ya kujiri miripuko ya mabomu Alkhamisi iliyopita, yumkini waliuawa na wanajeshi wa Marekani.
Kanali ya Russia Today imenukuu mashuhuda waliohojiwa na Shirika la Utangazaji la BBC wakisema kuwa, si kila aliyeaga dunia katika miripuko ya Kabul aliuawa kwa bomu, baadhi waliuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Marekani.
Ndugu ya mmoja wa wahanga wa mashambulio hayo aliyeuawa pamoja na mkewe katika Uwanja wa Ndege wa Kabul amesema wanandoa hao waliuawa kwa kupigwa risasi baada ya kuzuka tandabeluwa kufuatia kujiri miripuko hiyo.
Chanzo kingine cha habari kinasema, raia mmoja wa Kiafghani aliyekuwa akishirikiana na jeshi la Marekani aliuawa na askari hao. Habari zaidi zinasema kuwa, maiti ya Muafghani huyo ilipatikana na jeraha la risasi kichwani wala haikuwa na majeraha mengine.
Watu wasiopungua 170 waliuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa kufuatia miripuko miwili ya mabomu iliyotokea nje ya Uwanja wa Ndege wa Hamid Karzai mjini Kabul nchini Afghanistan Alkhamisi iliyopita.
Kundi la kigaidi la ISIS lilitangaza kuhusika na hujuma hiyo ambayo ni ya kwanza kutokea mjini Kabul tangu rais Ashraf Ghani aitoroke nchi; na mji mkuu huo wa Afghanistan kudhibitiwa na kundi la Taliban mnamo tarehe 15 Agosti.