Moscow: Tunataraji silaha za Wamarekani hazitatumika katika vita vya ndani Afghanistan
Mjumbe Maalumu wa Rais wa Russia katika Masuala ya Afghanistan ameeleza wasiwasi wake kuhusu idadi kubwa ya silaha zililizoachwa na wanajeshi wa Marekani huko Afghanistan na kusema kuwa kuna uwezekano Moscow ikashiriki katika kujenga upya uchumi wa nchi hiyo.
Zamir Kabulov amedokeza suala la kuondoka haraka wanajeshi wa Marekani huko Afghanistan na kuongeza kuwa, Moscow inataraji kuwa silaha ziliazoachwa na wanajeshi wa Marekani huko Afghanistan hazitatumika katika vita vya ndani vinavyoweza kushuhudiwa nchini humo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Kabulov amebainisha kuwa Moscow inazitaka nchi za Magharibi zisizuie fedha za viongozi wapya wa Afghanistan na wala wasisababishe matatizo zaidi kwa raia wa nchi hiyo.
Mwanadiplomasia huyo wa Russia amezungumzia pia mchakato wa kuondoka vikosi ajinabi huko Afghanistan na kueleza kuwa, viongozi wa Marekani wanataka wawe wamewaondoa wanajeshi wao huko Afghanistan ifikapo mwishoni mwa mwezi huu hata hivyo wakati huo huo hawawezi kuwaondoa nchini humo wale wote waliofanya kazi na wanajeshi hao.
Amesema Russia inaunga mkono wazo la kufanyika Mkutano wa Kimataifa wa kujadili ujenzi mpya wa Afghanistan.