Ahmad Masoud asisitiza kuendelea kupambana na kundi la Taliban
Ahmad Masoud, Kiongozi wa Waafghanistan wanaolipinga kundi la Taliban ametoa mwito wa kuendelezwa mapambano dhidi ya kundi hilo.
Ahmad Masoud, ambaye ni mwana wa Ahmad Shah Masoud, shujaa wa taifa wa Afghanistan amesema leo kwamba: "Hatutaacha katu kupambana kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, uhuru na uadilifu."
Mkoa wa Panjshir, ndilo eneo pekee ambalo bado halijadhibitiwa na Taliban; na Ahmad Masoud pamoja na Amrullah Saleh, makamu wa rais wa Afghanistan Ashraf Ghani aliyeitoroka nchi, pamoja na wapiganaji wao, wamezatiti ngome zao katika mkoa huo.
Vita na mapigano mkoani Panjshir baina ya wapiganaji wa Taliban na wapinzani wanaoongozwa na Ahmad Masoud yangali yanaendelea huku kila upande ukidai kusonga mbele.
Hayo yanajiri huku Fahim Dashti, msemaji wa vikosi vya wapiganaji wanaolipinga kundi la Taliban akitangaza jana Ijumaa kuwa wapiganaji 450 wa kundi hilo wameuawa na wengine 130 wamekamatwa mateka.
Kwa mujibu wa Dashti wapiganaji wa Taliban wamelazimika kurudi nyuma kutoka mkoa wa Panjshir.
Katika upande mwingine, msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid ametangaza kuwa, karibu asilimia 20 ya eneo la mkoa wa Panjshir inadhibitiwa na wapiganaji wa kundi hilo na kwamba wapiganaji wao wanasonga mbele kuelekea makao makuu ya mkoa huo.
Tarehe 15 Agosti, vikosi vya kundi la Taliban viliingia mji mkuu wa Afghanistan Kabul; na sambamba na kuingia vikosi hivyo, rais Ashraf Ghani aliitoroka nchi na hivi sasa amepatiwa hifadhi katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).../