Mashinikizo yazidi, Biden aamuru kuchapishwa nyaraka za tukio la Septemba 11
https://parstoday.ir/sw/news/world-i74292-mashinikizo_yazidi_biden_aamuru_kuchapishwa_nyaraka_za_tukio_la_septemba_11
Rais Joe Biden wa Marekani ametoa taarifa akiamuru kuchunguzwa nyaraka zinazohusiana na tukio la Septemba 11 mwaka 2001 kwa ajili ya kuondolewa nyaraka hizo katika hali ya usiri.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 04, 2021 22:21 UTC
  • Joe Biden
    Joe Biden

Rais Joe Biden wa Marekani ametoa taarifa akiamuru kuchunguzwa nyaraka zinazohusiana na tukio la Septemba 11 mwaka 2001 kwa ajili ya kuondolewa nyaraka hizo katika hali ya usiri.

Biden amesema katika taarifa hiyo kwamba, kuweka wazi nyaraka za tukio la Septemba 11 ilikuwa miongoni mwa ahadi zake kwenye kampeni za uchaguzi wa rais na kwamba sasa anataka kutekeleza ahadi hiyo. Agizo hilo la Rais wa Marekani linamtaka Waziri wa Sheria wa nchi hiyo, Merrick Garland na Mwanasheria Mkuu kuchapicha nyaraka zitakazotolewa katika usiri za tukio la Septemba 11 katika kipindi cha miezi sita ijao. 

Hatua hiyo ya Rais wa Marekani kwa hakika ni jibu kwa mashinikizo ya wananchi hususan familia za wahanga wa mashambulizi ya Septemba 11 ambazo kwa muda mrefu sasa zimekuwa zikitaka kuchapishwa na kuwekwa wazi nyaraka zote zinazohusiana na tukio hilo ili kufichua nafasi ya wahusika wote katika faili hilo hususan maafisa wa serikali ya Saudi Arabia. 

Agizo hilo la Biden pia limetolewa kabla ya kumbukumbu ya mashambulizi ya Septemba 11 na hapana shaka kuwa, katika kipindi hiki kutashuhudiwa matakwa mengi ya wananchi ya kuwekwa wazi zaidi wahusika wa mashambulizi hayo. Mtaalamu wa masuala ya siasa, Reza Mirabian anasema: "Faili la mashambulizi ya Septemba 11 ni moja kati ya masuala yatakayotumiwa kuzidisha mashinikizo kwa Saudi Arabia katika kipindi cha utawala wa Joe Biden."  

Mashambulizi ya Septemba 11

Katika upande mwingine inaonekana kuwa, kwa kutoa agizo hilo la kuchunguzwa nyaraka zinazohusiana na tukio la Septemba 11 mwaka 2001, Joe Biden anataka kupunguza malalamiko na ukosoaji wa ndani na nje ya nchi kuhusiana na kuondoka kwa fedheha na madhila kwa wanajeshi wa Marekani huko Afghanistan na kuzivutia upande wake fikra za Wamarekani; hasa kwa kutilia maanani kwamba, umaarufu wake umeshuka na kufika kiwango cha chini zaidi tangu aliposhika hatamu za kuiongoza Marekani.

Mwezi uliopita familia za wahanga wa mashambulizi ya Septemba 11 zilimwambia Joe Biden kwamba, hazitamkaribisha katika hafla ya kumbukumbu ya wahanga wa mashambulizi hayo ila pale atakapochapisha nyaraka na ushahidi wa serikali unaoweka wazi nafasi ya Saudi Arabia katika mashambulizi hayo.

Kwa sasa unapokaribia kutimia mwaka wa 20 tangu baada ya mashambulizi hayo yaliyofanyika mwaka 2001, familia za watu waliouawa katika hujuma hiyo zinavishinikiza vyombo vya sheria vya Marekani viweke wazi nyaraka zote za kuhusika serikali ya Saudia katika mashambulizi hayo. Kesi ya mojawapo ya mashtaka hayo imepiga hatua nzuri mwaka huu wa 2021 na maafisa wa Saudia wameitwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

Utawala wa Saudi Arabia daima umekuwa ukikanusha madai ya kuhusika katika mashambulizi hayo au hata kushirikiana na watu walioteka nyara ndege zilizotumiwa katika hujuma hiyo. Hata hivyo nyaraka za siri za serikali ya Marekani zinaonyesha kinyume chake na ndiyo maana familia za wahanga wa mashambulizi hayo zinashinikiza ili nyaraka hizo ziwekwe wazi kwa umma.

Kwa kutilia maanani masuala ya kisiasa, kiuchumi na jiografia ya kisiasa na vilevile mahusiano ya Marekani na Saudi Arabia, serikali zilizopita za Washington zikiwemo serikali za Barack Obama na Donald Trump zimefanya jitihada za kuikingia kifua Saudi Arabia kama mshirika mkuu wa Marekani katika eneo la Magharibi mwa Asia na kuficha nafasi na kuhusika kwake  katika mashambulizi ya Septemba 11. Hasahasa serikali ya Donald Trump iliikingia kifua sana Saudi Arabia na haikuwa tayari kuona uhusiano wa Washington na Riyadh ukiathiriwa na kadhia hiyo.

Trump na Bin Salman

Ripoti ya Kongresi ya Marekani iliyotolewa mwezi Juni mwaka 2016 kuhusu tukio la mashambulizi ya Septemba 11 ilisema waziwazi kwamba, 15 kati ya watu 19 walioshiriki kuteka nyara ndege zilizotumiwa katika mashambulizi hayo walikuwa raia wa Saudi Arabia. Suala hilo lilipelekea kupasishwa sheria ya JASTA katika Kongresi ya Marekani ambayo inazipa familia za wahanga wa mashambulizi ya Septemba 11 ruhusa ya kufungua mashtaka dhidi ya serikali na maafisa wa Saudia walioshirikiana na wahusika wa moja kwa moja wa mashambulizi hayo.

Hatua ya Kongresi ya kupasisha sheria ya JASTA kwa hakika ni kukiri kwamba, utawala wa Saudi Arabia unaunga mkono ugaidi. Sasa na baada ya Joe Biden kutoa agizo za kufichuliwa nyaraka zaidi za tukio la Septemba 11, inatarajiwa kuwa kutawekwa wazi mengi zaidi kuhusu nafasi ya maafisa wa Saudi Arabia katika tukio hilo. Hata hivyo hatupasi kusahau kuwa, sababu kuu ya kukwamishwa kesi hiyo katika kipindi chote cha miongo miwili iliyopita ni ushawishi wa  Saudia na Marekani katika faili hilo. Inaonekana kuwa, mara hii pia hali itakuwa hivyo hivyo licha ya agizo la Biden la kufanyika uchunguzi kuhusu nyaraka za tukio hilo.