Mpango wa Taliban wa kubadilisha katiba ya Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i74360-mpango_wa_taliban_wa_kubadilisha_katiba_ya_afghanistan
Mmoja wa wanachama wa Baraza la Uongozi la Taliban amesema kuna tofauti kubwa kati ya mfumo wa siasa wa zamani na wa sasa wa kundi hilo na kwamba siasa mpya za kundi hilo haziwezi kulinganishwa hata kidogo na za zamani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 06, 2021 20:48 UTC
  • Mpango wa Taliban wa kubadilisha katiba ya Afghanistan

Mmoja wa wanachama wa Baraza la Uongozi la Taliban amesema kuna tofauti kubwa kati ya mfumo wa siasa wa zamani na wa sasa wa kundi hilo na kwamba siasa mpya za kundi hilo haziwezi kulinganishwa hata kidogo na za zamani.

Akizungumza karibuni na shirika la habari la Iran Press, Jalaluddin Shinwari amesema msingi wa katiba ya Afghanistan ni Qur'ani, Suna, Ijmaa na Qias na kwamba marekebisho ya baadhi ya vipengee cya katiba ya hivi sasa sio takwa la Taliban pekee bali ni takwa la makundi yote ya kisiasa ya nchi hiyo.

Akijibu swali kuhusu nafasi ya wanawake katika katiba hiyo mpya amesema, Taliban imekuwa ikisema siku zote kuwa italinda haki za raia wote wa Afghanistan na kuwa kundi hilo halitaki chochote cha ziada kutoka kwa wanawake wa nchi hiyo bali ni kuwataka tu wazingatie vazi la stara la hijabu wanapokuwa hadharani, makazini na vituo vingine vya umma.

Huku akijibu swali kuhusu uhusiano wa baadaye wa Afghanistan na nchi jirani, Jalaluddin Shinwari amesema uongozi wa sasa wa nchi hiyo unataka kuwa na uhusiano mzuri na majirani zake wote na hasa, Pakistan, Iran na China. Dalili zilizopo zinaoonyesha kwamba Taliban inataka kubadilisha katiba ya Afghanistan kwa msingi wa mahitaji na matakwa yake binafsi. Hata hivyo Jalaluddin Shinwari, amesema takwa la kubadilishwa katiba ya Afghanistan sio la kundi hilo pekee bali ni la makundi yote ya kisiasa ya nchi hiyo.

Viongozi wa Taliban wakiwa na Jean Arnault (wa pili kulia), Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan

Kubadilishwa katiba ni moja ya matakwa muhimu yaliyofuatiliwa kwa nguvu zote na Taliban katika mazungumzo ya amani na serikali ya zamani ya Afghanistan huko Doha Qatar, mazungumzo ambayo hayakuwa na natija yoyote chanya bali hatimaye kundi hilo lilifanikiwa kuteka mji mkuu wa Afghanistan Kabul, mnamo tarehe 15 Agosti iliyopita, na kudhibiti mamlaka ya nchi hiyo baada ya serikali ya Rais Muhammad Ghani kusambaratika na kumlazimu kukimbia nchi.

Hata kama Jalaluddin Shinwari hakubainisha kundi hilo linalenga kufuta vipengee vipi katika katiba ya sasa ya Afghanistan, lakini kwa kuzingatia misimamo ya huko nyuma ya Taliban, ni wazi kuwa kundi hilo limeazimia kufuta vipengee vinavyohusiana na mfumo wa uongozi wa rais, uchaguzi na jamhuri na kuvibadilisha na mfumo wa kisiasa wa imarati ya Kiislamu.

Matamshi ya Jalaluddin Shinwari kuhusu haki za wanawake nchini Afghanistan yanaonekana kuzingatia wasi wasi na hofu ya jamii ya kimataifa juu ya vitendo vya huko nyuma vya kundi hilo dhidi ya wanawake.

Katika kipindi chao cha kwanza cha utawala Taliban waliwawekea wanawake vikwazo chungu nzima ambapo waliwazuia kusoma kwenye shule na vyuo vikuu na vilevile kuwakataza kujishughulisha na mambo mbali mbali katika nyanja za usanii, utamaduni na masuala ya kiraia.

Baada ya kundi hilo kufanikiwa tena kuchukua madaraka huko Afghanistan, wanawake wa nchi hiyo wameingiwa na wasi wasi mkubwa na kuwa huenda wakazuiwa kufanya shughuli zao za kila siku ambazo wamekuwa wakijihusisha nazo tangu miaka 20 iliyopita.

Rais Ashraf Ghani aliyekimbia nchi kufuatia hujuma ya Taliban

Pamoja na hayo lakini matamshi ya karibuni ya Jalaluddin Shinwari yanaonyesha kuwa kundi hilo sasa limebadili misimamo yake mikali ya huko nyuma ya kubana na kuwawekea wanawake vizingiti visivyofaa, na kwamba sasa wana uhuru wa kujishughulisha na mambo tofauti katika jamii alimuradi waheshimu na kuzingtatia vazi la hijabu.

Pamona na hayo, inaonekana kuwa utekelezwaji wa mitazamo mipya ya kisiasa ya Taliban, ikiwemo ya ubadilishaji katiba ya Afghanistan katika kipindi hiki cha utawala wao, utakabiliwa na changamoto kubwa na kuibua makele mengi nchini humo.